MBUNGE CHIKOTA ASHAURI IUNDWE TUME YA KUCHUNGUZA KUSHUKA KWA UZALISHAJI KOROSHO


Na Mwandishi Wetu, DODOMA

Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota, ameomba kuunda Tume huru ya kuchunguza kushuka kwa uzalishaji wa zao la korosho ndani ya miaka mitatu mfululizo licha ya jitihada za kupanua wigo wa kilimo cha zao hilo kwenye mikoa mbalimbali.

Akichangia jana mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa mwaka 2023/24, Mbunge Chikota alisema pamoja na jitihada za serikali za kuratibu upatikanaji wa pembejeo kuna mdondoko wa zao hilo.



“Napongeza serikali ya awamu ya sita kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuwekeza katika tasnia ya korosho, tumeona kwa miaka mitatu mfululizo, Serikali ikitoa pembejeo bure kwa wakulima wa korosho, tunaendelea kuishukuru Serikali.”

“Mwaka huu kuna mikataba yenye thamani ya Sh bilioni 340 ambayo imetolewa na nina matumaini pembejeo hizi zitafika kwa wakati na wakulima wa korosho watanufaika na pembejeo,”alisema Chikota.

Kadhalika, alisema pamoja na uwekezaji ulifanywa na serikali kwenye tasnia ya korosho bado kuna anguko la uzalishaji wa korosho nchini ambapo kwa kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2017/18, Tanzania ilifikisha uzalishaji wa tani 320,000.

“Lakini kwa masikitiko makubwa katika msimu uliopita uzalishaji umepungua hadi kufikia tani 160,000 pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa, ukiuliza Bodi ya Korosho hawana majibu ya uhakika na hata taasisi ya utafiti ya TARI Naliendele hawana majibu ya kutoshereza ya anguko kubwa na uzalishaji wa korosho,”alisema.



Alisisiza “Haiwezekani mikoa ya uzalishaji wa korosho imeongezeka, serikali imefanya uwekezaji wa kutosha lakini uzalishaji unazidi kuwa mdogo.”

Chikota alisema malengo ya Bodi ya Korosho mwaka huu ilikuwa ni kufikisha tani laki nne na Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kufikisha tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.

“Kwa anguko hili kuna kazi kubwa inayopaswa kufanywa ili kufikia malengo nashauri serikali kuunda tume hii huru yenye wataalamu kutoka nje ili kupata mawazo mapya,”alisema.

Aliomba watumie wataalamu wa nje na SUA ili kuangalia mfumo wa uagiziaji na udhibiti wa pembejeo kwa kuangalia ubora wake.

“Tusiendelee kuwatumia wataalamu wale wale wa TARI na Bodi ya Korosho watatuletea majibu yela yale tuliyoyazoea. Tupate timu mpya, ikiwezekana tuchukue uzoefu kutoka huko,”alisema.

Pamoja na hayo, Chikota aliishauri Serikali kuimarisha miundombinu ya barabara na reli ili kufungua mikoa ya kusini.

Pia alishauri Serikali kutekeleza mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma ili kuweza upatikanaji wa maji hatua ambayo itavutia wawekezaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post