SERIKALI YAAGIZA UCHUNGUZI MATUMIZI YA VINYWAJI VYA KUONGEZA NGUVU 'ENERGY DRINK'


SERIKALI imeiagiza Taasisi ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kufanya uchunguzi dhidi ya vinywaji vya kuongeza nguvu (Energy Drinks), ili kubaini kama vina madhara kiafya kama inavyodaiwa. 


Agizo hilo limetolewa leo tarehe 24 Aprili 2023 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kupitia akaunti yake ya Twitter, baada ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kutoa tahadhari kwa wananchi juu ya matumizi ya vinywaji hivyo ikisema kwamba sio salama.


Ummy amesema uchunguzi wa kisayansi utakapofanyika dhidi ya vinywaji hivyo, utaisaidia Serikali kuchukua hatua stahiki.


“Nimeielekeza Taasisi yetu ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu @NIMR_Tanzania kufanya utafiti zaidi kuhusu suala hili la matumizi ya #EnergyDrink na kutupa ushahidi wa kisayansi ili tuweze kuchukua hatua stahiki,” ameandika Ummy.


Vinywaji hivyo pendwa hasa kwa rika la vijana, vinadaiwa kuwa na visisimuzi vingi ambavyo vinaathiri afya ya binadamu hususan mfumo wa damu ambapo inadaiwa mtu anayetumia yuko katika hatari ya kupata tatizo la damu kuganda.


Hivi karibuni, JKCI ilitoa taarifa iliyoeleza kwamba, imemtibu kijana mwenye umri wa miaka 28, ambaye alipata madhara kiafya baada ya kutumia kinywaji hicho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments