KAMATI YA MIUNDOMBINU YAITAKA SERIKALI KUWEKA MKAKATI WA KUTOA ELIMU YA TEHAMA


Na Mwandishi wetu wa WHMTH, Dodoma.


Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetakiwa kuhakikisha inatenga bajeti mahususi kwa ajili ya kutoa elimu ya TEHAMA nchini.

Rai hiyo imetolewa na Mhe Selemani Kakoso (Mb) ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati wa kikao cha kamati kilichohusisha Wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya hanari kilichofanyika leo terehe 27 Machi 2023 katika Ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma.

Mhe Kakoso ameeleza kuwa ulimwengu wa utandawazi umesababisha kusambaa kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hususani matumizi ya kompyuta na viambata vyake na kuitaka Wizara hiyo kuhakikisha inatenga bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa ajili ya kazi hiyo. 

Amesema kuwa "Kuwe na mkakati wa maboresho na mpango wa kuhakikisha kuwa elimu ya TEHAMA inaenezwa nchini maana sote lazima tukubaliane kuwa TEHAMA ndio ulimwengu wa sasa.”

Mhe Kakoso amesema kuwa endapo mapato ya Serikali yatakuwa ni kidogo kuna kila sababu ya kutafuta fedha mahali popote ili kuhakikisha mapinduzi ya TEHAMA yanapatikana nchini.

"Mimi nawahakikishia kuwa bila kujenga vijana wenye teknolojia bora nchi yetu haitakuwa salama, TEHAMA ndio mwarobaini wa maendeleo ya nchi yetu na Dunia nzima imeelekea huko", amesisitiza Mhe Kakoso.

Kadhalika, Mhe Kakoso amepongeza kazi zinazofanywa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kufanya maboresho na usimamizi madhubuti wa miradi ya mawasiliano katika maeneo mengi nchini.

"Nawahakikishia kuwa kama tungetegemea mfumo wa makampuni pekee kusingekuwa na mawasiliano ya kutosha. Minara mingi imezidiwa hivyo ni vizuri kuendelea kufanya maboresho ili kuondoa changamoto zozote za mawasiliano", ameeleza Mhe Kakoso.

Akijibu baadhi ya hoja za Wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu changamoto za mawasiliano mipakani, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb) amesema kuwa lengo la Serikali ni kuimarisha huduma ya mawasiliano katika mipaka ya Tanzania kwa sababu mipaka hiyo inabeba taswira ya uchumi wa nchi na pia masuala ya usalama na kuwapatia fursa Watanzania kuona kile ambacho kinatokea ndani ya nchi yao.

Mhandisi Kundo amesema kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya mipakani wamekuwa wakitumia gharama kubwa kupata huduma za mawasiliano kupitia huduma ya ‘roaming’ kutokana na mwingiliano wa mawasiliano na kupelekea kuchangia mapato ya nchi jirani kupitia huduma hiyo.

Ameeleza kuwa, Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) limeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata haki ya kupata habari kwa kufikisha usikivu wa redio zake nchi nzima.

Kuhusu mawasiliano, Naibu Waziri Kundo amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini kwa lengo la kutatua changamoto ya mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuvutia uwekezaji na kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi.

Amesema kuwa ni dhahiri kuwa huduma za mawasiliano ni za msingi katika maisha ya wananchi kwa vile zinagusa nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Pia, mawasiliano yanawezesha na kuhimili sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, kilimo, uwekezaji na biashara na kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa moja kwa moja kupitia sekta hizo.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments