FISI AUA NG'OMBE, AJERUHI WANAKIJIJI 10 GEITANa Rose Mweko - Geita
WATU 10 wakiwemo watano wa familia moja katika kijiji cha Nyamarimbe, kata ya Nyamarimbe tarafa ya Busanda wilayani Geita wamenusurika kufa baada ya kushambuliwa na fisi mmoja kijijini hapo.


Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Berthaneema Mlay amethibitisha alipozungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa tukio  hilo limetokea jioni Machi 29, 2023.

ACP Berthaneema alisema kabla ya kufanya shambulizi hilo, watoto wawili walinusurika kushambuliwa na fisi huyo wakiwa machungani ambapo walikimbia kutoa taarifa na fisi huyo kuua ng’ombe mmoja.


“Waliojeruhiwa ni 10 ambao walipata huduma ya kwanza katika kituo cha afya cha Nyamarimbe, na baadaye walihamishiwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita kwa ajili ya matibabu zaidi.


“Wananchi watano ni watu wa familia moja kwa maana kwamba kuna mama na watoto wake wawili wa kike na mmoja wa kiume pamoja na kaka yake”, alisema Kamanda na kuongeza;

“Baada ya wananchi kupata taarifa wakawa wamekuja, yule fisi alitoka kule vichakani baada ya kusikia sauti za watu, akaanza kuvamia wale wananchi.

“Kwa hiyo kila anayekuja kumuokoa mwenzake anashambuliwa na yule fisi, lakini tulipopata zile taarifa kama jeshi la polisi mkoa wa Geita, tuliwasiliana na watu na TFS pamoja na uongozi wa wilaya.”

Kamanda Berthaneema alisema askari wa vituo vidogo vya polisi karibu na eneo la tukio waliagizwa kwenda kukabiliana na fisi huyo ambapo walimshambulia na kufanikiwa kumuua kwa risasi tatu.


“Rai yetu kwa wananchi waendelee kuchukua tahadhari wanapokuwa mashambani, na asiwe mmoja, kati yao angalau wawe wawili, watatu, ili kuweza kunusuru maisha yao anapotokea mnyama mkali.”


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita, Dk Mfaume Kibwana alithibitisha kupokea majeruhi hao 10 na kueleza kati yao wanne walitibiwa na kuruhusiwa na sita kulazwa kwa matibabu.


“Walikuwa na majeraha madogomadogo kwenye mikono na miguu, walipewa huduma kitengo cha dharura, na jana (juzi) tulifanikiwa kuruhusu watu wanne, na sita walilazwa kupatiwa huduma wodini.”

Majeruhi wa tukio hilo, Maneno Petro (35) na Enock Bahati (31) walisema walikumbana na adha ya kushambuliwa na fisi huyo wakati wakiendelea kumusaka ili wamuue baada ya kuarifiwa.

Chanzo - Theprofiletv blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post