BABA AKAMATWA TUHUMA ZA KULAWITI WATOTO WAKE WA MIAKA 8 na 11 SHINYANGA MJINI


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linachunguza tukio linalomhusisha mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka zaidi ya 35 kwa tuhuma za kuwalawiti watoto wake wawili wenye umri wa miaka 8 na 11 wanafunzi wa shule ya msingi Mapinduzi B, iliyopo kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi amethibitisha mwanaume huyo kukamatwa kwa ajili ya uchunguzi.

Kamanda Magomi amesema upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Akizungumzia tukio hilo Kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Kambi Butete amesema Februari 22 Mwaka huu majira ya saa tano asubuhi watoto hao walifikishwa katika Hospitali hiyo na kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari ambapo majibu ya vipimo vyao yamekabidhiwa kwa vyombo vya usalama kwa ajili ya hatua za kisheria.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mapinduzi B, Hassan Hemed ambaye ameeleza namna alivyopokea taarifa za tukio hilo, na kusema kuwa kushamiri kwa matukio hayo inachangiwa na wazazi na walezi kutowajibikia jukumu la malezi bora na makuzi kwa watoto.

‘Hizi taarifa za hawa watoto wawili nilizipokea kwa kuletewa na watu ambao wao wanasema ni wanaharakati ndiyo waliniletea hawa watoto saa sita usiku asubuhi nikaenda kwa hawa watoto mpaka wanapoishi mpaka ndani kwao ni kweli wanalala chumba kimoja na baba yao mzazi", amesema Mwalimu Hemed.

Taarifa za kulawitiwa kwa watoto hao ziliripotiwa kwa Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Mapinduzi B, usiku wa Februari 22, Mwaka huu 2023.

Via Misalaba blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments