JUMUIYA YA WAZAZI MKOA WA DAR ES SALAAM YAPONGEZWA KUANDAA MAFUNZO YA UONGOZI KWA VIONGOZI WAKE


Na Mwandishi Wetu

NAIBU Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Balozi Rajab Luwhavi ameipongeza Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuandaa mafunzo maalumu ya viongozi wa jumuiya hiyo yaliyoanza kutolewa kwa Kamati ya utekelezaji.

Balozi Luwhavi ametoa pongezi hizo leo Januari 13,2023 jijini Dar es Salaam mbele ya washiriki wa mafunzo hayo yaliyoratibiwa na jumuiya hiyo chini ya Uongozi wa Mwenyekiti wake Khadija Ally baada ya kutembelea Kambi ya mafunzo hayo ya siku tatu yanayofanyika Kigamboni,Jijini Dar es Salaam.

Amesema kwamba amevutiwa na mafunzo hayo na yameonesha mwanzo mpya wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwamua kuwapatia mafunzo hayo viongozi wake.

“Nampongeza Mwenyekiti Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam Khadija Ally kwa kuandaa mafunzo haya.Hakujipa muda wa kusherehekea nafasi aliyoipata baada ya kuchaguliwa ameamua kuandaa mafunzo hayo huku akitumia nafasi hiyo kukumbusha mambo ya msingi yanayohusu Chama hicho na jumuiya zake'',amesma Balozi Luwahi.

Amesema moja ya changamoto iliopo ni zana ya kuamini wanaopaswa kuelimishwa ni wale walioko chini kabisa,la hasha huyu Mwenyekiti mmepata mpya kabisa na maalum, ameanza kujifunza yeye na Kamati yake ya utendaji kwanza,na kwamba anampongeza Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, kwa sababu mtazamo wake sio mtazamo wa viongozi wa sasa .

''Mkoa wa Dar es Salaam ni namba moja kwa kila kitu, namba moja kwa ukubwa wake maana ndio unaongoza kwa idadi ya watu Tanzania, lakini ndio namba moja kwa nguvu zake kiuchumi,ndio mlango mkubwa wa kupokea na kutoa wageni kwenye nchi yetu, unapopata uongozi Mkoa wa Dar es Salaam ni tofauti na unapopata uongozi katika mkoa mwingine,Kwanini ni kwasababu ya mazingira ya mkoa wenyewe kwa hiyo nampongeza sana kwa mwanzo aliounesha wa kuandaa mafunzo haya kwa kamati yake ya utekelezaji ''amesema Balozi Luwhavi.

“Nampongeza yeye kwasababu hakujipa muda wa kusherehekea nafasi aliyoipata baada ya kuchaguliwa, amekiwahi hata chama chenyewe, tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu na maarifa , afya njema na umri mrefu zaidi ili atutumikie zaidi kwenye chama chetu, lakini niwapongeze ninyi nyote kwa kuchaguliwa.

Kuhusu jumuiya ya wazazi amesema kwa mujibu wa historia ndio jumuiya kubwa yenye lengo la kuwanganisha wazazi wote na kuwa mwanachama wa jumuiya ya wazazi sio lazima uwe mwanachama wa CCM.

“Katiba ya CCM haijawazuia kuwa mwanachama wa CCM kama haujaingia kwenye jumuiya wala haijasema kwa mtu anayependa kuwa mwanachama wa jumuiya ya wazazi peke yake akaridhika akawa mwanachama wa CCM isipokuwa tu ukitaka kugombea uongozi utakaokuingiza kwenye vikao vya Chama hicho basi sharti lake lazima uwe mwanachama wa CCM.

” Ndio maana huko nyuma tulitenganisha suala la itikadi na kuwaunganisha watu,kwasababu jukumu la kwanza la jumuiya ya wazazi ni kuwaunganisha wazazi wote chini ya uongozi mmoja, jukumu lake la pili ndio la kwenda kwenye uanachama.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam Khadija Ally amewaomba waliopata nafasi ya kushiriki kwenye mafunzo ya uongozi kuwa wasikivu ili nao waweze kuacha alama bora na alama ya uongozi bora uliotukuka.“Tuwe viongozi ambao tutaishi na hata tutakapokufa tutaacha alama na kuwa mfano kwa wengine.

Aidha amesema kupitia mafunzo ya uongozi yanayotolewa kwa viongozi hao kuna mambo mengi wamejifunza na washiriki wameonesha kubeba yale yote yaliyoelezwa na wakufunzi huku akitumia nafasi hiyo kueleza wameingia kwenye mafunzo hayo kama wajumbe lakini watatoka kama viongozi .“Dhana ni ile ile ,Chama chetu ya Mapinduzi kimekuwa tanuru la kutoa viongozi.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments