NAULI ZA MABASI YA MWENDOKASI, BAJAJI, TEKSI MTANDAO NA PIKIPIKI ZAONGEZEKA

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini nchini (LATRA) imetangaza nauli mpya za mabasi ya mwendokasi yanayofanya kazi zake jijini Dar es Salaam huku ikijiandaa kupanga nauli za treni ya mwendokasi (SGR).

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA),CPA Habibu Suluo ametangaza nauli hizo Januari 3, 2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari.Amesema, nauli hizo zimeongezeka kwa shilingi 100 kutoka nauli za zamani.

CPA Suluo amesema, mabadiliko hayo ni kwa mujibu wa sheria na yamepitishwa na Bodi ya Wakurugenzi baada ya kupokea maoni kuhusu nauli katika maeneo hayo.


Amesema, nauli ya mabasi ya mwendokasi kwa njia kuu ni shilingi 750 kutoka shilingi 600, njia ya mlisho ni shilingi 500 kutoka shilingi 400, njia ya mlisho na njia kuu ni shilingi 900 kutoka shilingi 800 na njia ya Kimara kwenda Kibaha ni shilingi 700 badala ya pendekezo la DART la shilingi 1,200.

CPA Saluo amesema, mapendekezo hayo ni kwa mujibu wa sheria, lakini kama kuna mdau yeyote ana malalamiko au hakubaliani nayo anakaribishwa kupeleka malalamiko yake ndani ya siku 14.

Wakati huo huo, nauli za teksi mtandao zinazobeba abiria wanne nauli itakuwa shilingi 3,000 hadi shilingi 4,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama kuna safari nyingine toka hapo nauli itaongezeka kwa shilingi 800 hadi shilingi 1,000 kwa kilomita moja na safari inapokutana na vikwazo kama foleni nauli ya ziada itaongezeka kwa shilingi 80 hadi shilingi 100 kwa dakika.

Amesema, kwa upande wa magari yanayobeba abiria sita nauli elekezi ni shilingi 4,000 hadi shilingi 5,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama kutakuwa na safari ya ziada toka ya awali nauli itaongezeka kwa shilingi 1,000 hadi shilingi 1,200 kwa kilomita moja na vinapotokea vikwazo kama foleni nauli itaongezeka shilingi 80 hadi shilingi 150 kwa dakika.
Pia smesema, kwa nauli za pikipiki ya kubeba abiria wawili nauli elekezi itakuwa shilingi 1,000 hadi shilingi 1,500 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama safari itaongezeka kutoka hapo nauli itaongezeka kwa shilingi 300 hadi shilingi 400 kwa kilomita moja na kama kutakuwa na vikwazo kama foleni nauli itaongezeka shilingi 50 hadi shilingi 70 kwa dakika.

Amesema, kwa upande wa nauli za pikipiki mtandao zinazobeba abiria wasiozidi watatu ni shilingi 2,000 hadi shilingi 2,500 kwa safari isiyozidi kilomita moja na safari ya ziada itakayongezeka nauli itaongezeka kwa shilingi 500 hadi shilingi 600 kwa kilomita moja na kama kutakuwa na vikwazo njiani kama foleni nauli itaongezeka kwa shilingi 70 hadi shilingi 90 kwa dakika moja.

Katika hatua nyingine, CPA Suluo amesema, bado wapo kwenye vikao vya masikilizano na wadau kuhusu nauli za treni ya mwendokasi (SGR) na bei kamili ya nauli hizo zitatangazwa mwezi ujao baada ya kuwasili kwa mabehewa nchini.

Aidha, kuhusu tiketi mtandao kuandika jina abiria, CPA Suluo amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanazingatia hilo ili ajali inapotokea waweze kutambulika kirahisi kwa hatua za haraka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments