MLOGANZILA YAANZISHA HUDUMA YA KUWEKA PUTO KWENYE TUMBO LA CHAKULA KUSAIDIA WENYE UZITO MKUBWA KUPUNGUA.


*******************

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imezindua huduma mpya ya kuweka puto maalumu kwenye tumbo la chakula kwa watu wenye uzito uliopitiliza (intragastic ballon) ambayo itasaidia kupunguza nafasi kwenye tumbo la chakula hivyo kusababisha mtu kula kidogo jambo ambalo litapelekea kupungua uzito.

Akizindua huduma hiyo leo Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema, Mloganzila ndio Hospitali ya kwanza ya umma Tanzania kutoa huduma hiyo hivyo amewapongeza wataalamu kwa kufanikisha jambo hilo" amesema Prof. Janabi

“Hadi leo tumefanya kwa watu 3 na kuna zaidi ya watu 12 ambao wanahitaji huduma hiyo, wanaotakiwa kupatiwa huduma hii ni wale wenye uzito uliopitiliza ambao ni kuanzia kilo 100.

Kuhusu gharama za huduma hiyo , Prof. Janabi amefafanua kwamba kwa Mloganzila inagharimu TZS 3.5 Mil hadi TZS 4 Mil wakati nje ya nchi ni zaidi ya TZS 15 Mil.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Eric Muhumba amesema huduma ya kuweka puto hufanyika kwa dakika 20 ambapo hufanyika kwa kutumia mashine ya Endoscopia (Endoscopy Mashine) hivyo haihusishi upasuaji wa aina yoyote.

Dkt. Eric ameongeza kuwa puto likishawekwa tumboni hukaa kwa muda kati ya miezi sita hadi nane ndipo hutolewa na baada ya hapo mtu huyo atakuwa ameshajenga utamaduni wa kula kidogo hivyo atakuwa amepuguza uzito wa kutosha.

Pia Dkt. Eric ameishauri jamii kufanya mazoezi na kula chakula kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa lishe ili kuwa na afya bora na kuepuka kupata uzito uliopitiliza ambao unasababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari, magonjwa ya moyo na kiharusi.

Naye, Mjumbe wa Kamati ya Utalii Tiba (Medical Tourism) Bw. AbdulMarik Mollel ameipongeza MNH-Mloganzila kwa kuzindua huduma hiyo ambayo itafungua milango kwa watu kutoka nchi jirani kuifuata kwa kuwa ni salama na gharama zake ni nafuu hivyo kusaidia kuitangaza Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments