WANANCHI MWAMALA WATAKA WATUMISHI ZAHANATI YENYE WATUMISHI WAWILI...NYINGINE INA NESI TU


Mwandishi wa habari Kadama Malunde (kulia) akizungumza na wananchi wa kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (Wengine hawapo pichani).
Afisa Mtendaji wa kata ya Mwamala Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga , Suzana Kayange akizungumza na Malunde 1 blog


Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Wakazi wa kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wameiomba serikali kuongeza idadi ya watumishi katika zahanati ya Kijiji cha Bugogo yenye mtumishi  mmoja (Nesi pekee) na Mwamala B yenye watumishi wawili tu hali ambayo inasababisha changamoto kwa wananchi wanapokwenda kupata huduma za matibabu.

 

Wakizungumza na Malunde 1 blog kwa nyakati tofauti wakazi wa kata hiyo wamesema upungufu wa watumishi katika zahanati ya Mwamala B na Bugogo unasababisha wananchi hususani akina mama na watoto kutumia muda mrefu wakisubiri huduma za matibabu na wakati mwingine kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu nje ya kata hiyo.

 

Pia wameiomba serikali ijenge kituo cha afya au kuongeza huduma kwenye zahanati zilizopo kama vile huduma za upasuaji ili kuwapunguzia adha akina mama wajawazito kusafiri hadi Samuye au Shinyanga mjini kufuata huduma za afya pindi wanapohisi watajifungua kwa njia ya upasuaji.

 

 “Watumishi wa afya hawatoshi, vitanda na vyumba vya kujifungulia kwa akina mama havitoshi,akina mama tunakosa pa kujifungulia, uchungu ukiwahi unajifungulia chini”,ameeleza Bi. Martha Tungu.


Bw. Madale Nyewe amesema kufuatia changamoto ya upungufu wa watumishi hao wachache waliopo wanaelemewa na wagonjwa na wakati mwingine  kutofanya kazi siku za Jumamosi na Jumapili, wagonjwa wanalazimika kwenda Samuye, Nhelegani au Shinyanga mjini kupata huduma za matibabu.

“Kama daktari ni mmoja, nesi mmoja tu na idadi ya wagonjwa ni wengi mimi naumwa halafu wakati mwingine hawapo kinachotokea ni nini?... Ukiona hivyo unajiongeza tu unaenda kupata matibabu Mjini Shinyanga, tunaomba serikali ituongezee watumishi wa afya”,amesema Bi. Justina Mihayo.

 

“Tulilomba bhize bhanesi, bhize Bhaganga, Ihaha Nesi omo doo, Nganga omo doo gede wa bhugota, yaya lulu (Tunaomba waje manesi, waje waganga, sasa hivi ni nesi mmoja tu, daktari mmoja tu kama wa dawa, hii si sawa)”,amesema Bi. Kang’wa Cherehani.


“Tunataka serikali ilete watumishi wa afya kwenye zahanati zetu ili tupate huduma bora…hawa watumishi waliopo wanafanya kazi zaidi ya uwezo wao, wakati mwingine wanachoka tu kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa, serikali ituhurumie kwa kweli”,ameongeza Bw. Nkende Mabula na Masesa Masele.


Afisa Mtendaji wa kata ya Mwamala Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga , Suzana Kayange amesema ni kweli zahanati ya kijiji cha Mwamala B  ina watumishi wawili pekee na Bugogo yupo mtumishi mmoja baada ya mtumishi mmoja kufariki dunia.

 

Ameongeza kuwa kata hiyo yenye zaidi ya wananchi 10,000 kaya zaidi ya 1000 ina vijiji vinne ambayo ni Bugogo, Mwamala B, Bunonga na Ibanza ambapo katika kijiji cha Bunonga majengo ya zahanati yapo usawa wa renta, zahanati ya kijiji cha Ibanza majengo yapo usawa wa madirisha.


“Majengo haya ya zahanati yamejengwa kwa nguvu za wananchi, tumeiandikia serikali kuu na halmashauri na wadau watusaidie kumalizia ujenzi wa zahanati hizi ili kuwasogezea huduma za matibabu wananchi”,amesema Kayange.

 

“Kutokana na changamoto hii wananchi wa kijiji cha Ibanza  wanaenda Mwamala kupata huduma za matibabu na wananchi wa kijiji cha Bunonga wanaenda zahanati ya Bugogo. Kulingana na idadi kubwa ya wananchi watumishi wanahitajika kwa wingi ,wanatakiwa 15 kila zahanati”,ameeleza Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwamala.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dkt. Nuru Yunge amekiri kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa watumishi kwenye zahanati nyingi katika halmashauri hiyo.


"Tuna changamoto, kuna zahanati nyingi tu zina mtumishi mmoja mmoja, tunaangalia namna ya kufanya Re- alocation kwa watumishi ndani ya halmashauri. Hiyo zahanati ya Bugogo yenye mtumishi mmoja tutapeleka mtumishi, ni nesi tu yupo pale, daktari alifariki dunia. Sasa hivi tunatafuta kwanza mtumishi wa kupeleka pale zahanati ya Bugogo",amesema Dkt. Yunge. 


"Ili kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi kwenye zahanati tunachofanya tunaangalia sehemu ambayo ina nafuu, tunapeleka sehemu zenye changamoto kwa sababu hatuna ajira mpya, ajira mpya tulipata watumishi 38 na wengi walipangiwa kwenye hospitali ya wilaya na vile vituo vipya vinavyofunguliwa",ameongeza Dkt. Yunge.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments