11 WAKAMATWA KWA MAKOSA YA KIMTANDAO..WAMO WANAOPOST UJINGA KWENYE ONLINE TV

 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI


JESHI LA POLISI TANZANIA


22 Desemba 2022

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA 11 MAKOSA YA KIMTANDAO

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya   Dar es Salaam  kwa kushirikiana na timu maalum ya kuzuia na kupambana na makosa ya  mtandao  limewakamata watuhumiwa  11 wa makosa  ya kimtandao  kufuatia  ufuatiliaji  mkali unaoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi na Timu hiyo  Maalum.


Katika hatua hiyo Jeshi la Polisi na timu hiyo, limemkamata Alex Magoti (26) Mkazi wa Tabora Mjini na wenzake nane kwa tuhuma za kumiliki luninga za mtandaoni na akaunti za mitandao ya kijamii ambazo zimekuwa zikitumika kusambaza taarifa za uongo au uzushi kuhusu, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wakuu wa Serikali.


Watuhuhumiwa hao wamekuwa wakiweka taarifa zao za uzushi, uongo na upotoshaji kwenye luninga za mtandaoni zinazotambulika kwa majina ya BSUN Online TV, GATTU Online TV, TAMUTAMU online TV, KILIMANJARO online TV na nyinginezo. Mfano wa taarifa hizo ni kama “Rais Samia akosoa vikali utawala wa Rais JPM, aanika ukatili aliofanya (haukubaliki hata kidogo)”IMEVUJA VIDEO, MBOWE APEWA SHAVU…!”, “DENI LA TAIFA LAIBUA MAZITO MWIGULU KUTUMBULIWA…!”, “GHAFLA MKE WA MAGUFULI AFA…!”, “ITAKUTOA MACHOZI UKWELI WOTE KIFO CHA MAGUFULI”


Pia, Jeshi la Polisi limemkamata, Joseph Mzava (19) mkazi wa Kinondoni Dar es Salaam, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo cha Biachara Dar es Salaam (CBE), kwa tuhuma za kujinasabisha kuwa yeye ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na  kufanikiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia mtandao kwa kutumia laini za simu zenye usajili usio na majina yake.


Jeshi la Polisi pia limemkamata LI NAIYONG (48) raia wa China, ambaye anatuhumiwa kujihusisha na shughuli za kuingilia mfumo wa mawasiliano kinyume na taratibu za nchi, na kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Shilingi Milioni Mia mbili ishirini na moja laki moja sitini na tatu na mia sita (Tshs 221,163,600)


Mtuhumiwa huyo amekuwa akituma vifaa visivyo rasmi kuwaunganisha watu kwa simu kufanya mawasiliano nje ya nchi kinyume na sheria za mmlaka ya mawasiliano Tanzania. 

Watuhumiwa hao wamekutwa wakiwa na vifaa mbalimbali ambavyo wanavitumia kufanya uhalifu huo, vifaa hivyo ni:


  1. 1. Simu za mkononi 23
  2. 2. Laini za Simu 437 za makampuni mbalimbali ya huduma za simu zenye usajili wa watu tofauti tofauti.
  3. 3. Kompyuta Mpakato 6
  4. 4. Sim Box 5
  5. 5. Routers 3
  6. 6. Power Bank 1


Aidha, Jeshi la Polisi linatoa rai kwa Wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii, pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari na sheria zinazohusika kuepuka kuchapisha taarifa  za uongo na zile zitakazo zua taharuki kwa umma, Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa mtu/watu wote watakao vunja sheria, kanuni na miongozo inayoelekeza matumizi sahihi ya mitandao.


Imetolewa na

Muliro J. MULIRO - ACP

Kamanda Kanda Maalum ya Polisi 

Dar es Salaam


 www.polisi.go.tz 

www.twitter.com/tanpol

www.facebook.com/Polisi Tanzania www.instagram/polisi.tanzania  

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments