GGML, RAFIKI SURGICAL MISSION WATOA ‘AMBULENSI’ MBILI GEITA

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo (katikati) akikata utepe katika hafla ya kukabidhi magari mawili ya kubebea wagonjwa yaliyotolewa na Kampuni ya GGML na Shirika la Rafiki Surgical mission kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita mkoani Geita. Pamoja naye ni Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong (kulia) na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita, Dk. Modest Buchad Rwakahemula (kushoto).


NA MWANDISHI WETU, GEITA

KATIKA kuimarisha mahusiano mazuri baina ya Serikali na jamii zinazoizunguka kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) na Taasisi ya Rafiki Surgical Mission kutoka Australia wametoa msaada wa magari mawili ya kubeba wagonjwa kwa halmashauri ya wilaya ya Geita mkoani Geita.


Akizungumza katika hafla ya makabidhiano jana katika eneo la Nzera mkoani Geita, Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Terry Strong alisema GGML kushirikiana na Shirika la Rafiki Surgical mission wameamua kutoa magari hayo ili kuokoa maisha ya wagonjwa wengi katika halmashauri ya wilaya ya Geita mkoani Geita.


“Halmashauri ya Wilaya ya Geita iliomba magari mawili ya kubebea wagonjwa kutoka GGML kwa ajili ya kusaidia jamii ya eneo hilo kwa sababu baadhi ya wagonjwa walikuwa wakipata rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Geita ambayo iko mbali na Nzera na maeneo mengine ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita.


“GGML na Rafiki Surgical Mission walijibu vyema ombi hilo kwa sababu ni washirika wazuri wa maendeleo ambao wanasaidia miradi ya afya katika kipindi cha miaka 20 iliyopita,” alisema na kuongeza kuwa GGML na Rafiki Surgical Mission wamekuwa na ushirikiano mkubwa tangu mwaka 2000 kupitia upasuaji wa mdomo sungura na zaidi ya wagonjwa 1700 wamenufaika na mpango huo.


Terry alieleza kuwa GGML ilitumia zaidi ya Sh bilioni tano kusaidia miundombinu ya afya na usambazaji wa vifaa tiba kwa kipindi cha miaka 20 ya uendeshaji wake mkoani Geita.


GGML ilisaidia ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Geita, ujenzi, na ukamilishaji wa vituo vya afya zaidi ya 10 katika Mji wa Geita, ujenzi wa vituo vipya vya afya vinne, uboreshaji wa kituo cha afya cha Kasota na ukamilishaji wa vituo vingine vya afya na usambazaji wa vifaa tiba vya vituo vya Katoro & Bukoli vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita.


Akizungumza katika halfa hiyo kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo alisema msaada wa GGML umekuja wakati muafaka kwa sababu utaokoa maisha ya wagonjwa katika halmashauri ya wilaya ya Geita.


Aliwataka wadau wengine wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kushirikiana na Serikali ili kukabiliana na changamoto za kiafya mkoani Geita.


“GGML imekuwa mshirika mzuri katika kusaidia miradi mbalimbali ya afya mkoani Geita na Tanzania kwa ujumla. Mwaka jana, GGML ilitoa hadubini mpya kabisa kusaidia mapambano dhidi ya TB katika maeneo ya Madini Geita “alisema na kuongeza kuwa GGML imekuwa ikiendesha programu tofauti za afya kwa kushirikiana na Serikali kutatua changamoto za afya mkoani Geita.


Alisema tangu kuanzishwa kwa GGML imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Serikali, hususan Halmashauri za Wilaya na Miji ya Geita kusaidia miradi mbalimbali endelevu ya jamii mkoani Geita.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post