ZAIDI YA WAHANDISI 3500 KUSHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA WAHANDISI NCHINI

 
Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini Mha.Bernard Kavishe akizungumza na waandishi wa Habari juu ya maadhimisho ya siku ya wahandisi nchini itakayofanyika tarehe 22 - 23 Septemba 2022 Jijini Dodoma.

Na Dotto Kwilasa, DODOMA.

MAADHIMISHO ya siku ya wahandisi nchini yanatarajiwa kufanyika kesho tarehe 22 - 23 Septemba 2022 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma huku Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dodoma leo Msajili wa Bodi ya Wahandisi (ERB), Eng. Benard Kavishe, amesema maandalizi kwa ajili ya maadhimisho hayo yamekamilika na kwamba takriban wahandisi 3500 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki.

Eng. Kavishe amesema kuwa maadhimisho hayo yatawawezesha wahandisi kuuonesha umma nini wahandisi wa Tanzania wanaweza kufanya katika kuleta maendeleo ya nchi na kukuza uchumi na kuwawezesha wahandisi kuonesho ubunifu wa teknolojia mpya zinazotumiwa na wahandisi.

"Hii pia itakuwa fursa kwetu kuwatambua na kuwapongeza wahandisi wanaofanya vizuri katika kazi zao na kuwapongeza wanafunzi toka vyuo vikuu waliofanya vizuri katika kozi za uhandisi,"amesema 

Pamoja na hayo amesema takriban wahandisi 400 watakula kiapo cha utii na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taaluma na hivyo kuuwezesha umma kujenga imani kwa wahandisi na kuthamini kazi za kihandisi.

"Maadhimisho ya siku ya wahandisi mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Ubunifu na Uendelezaji wa Ujuzi katika Kuimarisha Maendeleo Endelevu ya Uchumi wa Taifa: mtazamo wa kihandisi”amesisitiza

Naye Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo Eng. Benedict Mukama, amesema tayari wahandisi kutoka nchi za Kenya, Uganda na Zambia wameshawasili nchini kuungana na wahandisi wa Tanzania.

"Kuna wengine hawatapata nafasi ya kuungana nasi hapa Ila watashiriki kupitia mitandao wa zoom ili kuwezesha maadhimisho kufuatiliwa Kwa makini na watu wengi zaidi duniani,"amefafanua 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post