RATIBA YA KUFUNGULIWA SHULE IPO PALE HAKUNA MAELEKEZO MENGINE : WAZIRI MKENDA

 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda


Na Mathias Canal ,PEMBA. 

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amekanusha taarifa za uzushi zinazotolewa na baadhi ya mitandao ya kijamii kuhusu tarehe ya shule kufunguliwa kuwa ni 21,Septemba 2022 na kueleza kuwa si sahihi na hakuna muongozo wala maelekezo hayo.

Prof. Mkenda amesema hayo leo  3, Septemba,2022 wakati akizungumza na wajumbe wa Bodi ya skuli ya Ole Sekondari iliyopo katika mkoa wa Kusini Pemba wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Zanzibar huku akieleza kuwa taarifa hizo zina lengo la kuichafua sekta ya elimu nchini.

Waziri Mkenda ameeleza kuwa ratiba ya kufunguliwa shule ipo vilevile kwa mujibu wa waraka wa elimu Na. 2 wa mwaka 2022 kuhusu mihula ya masomo uliotolewa na Kamishna wa elimu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Lyabwene Mtahabwa.

"Kuna taarifa imeenea katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikieleza kuwa shule zitafunguliwa tarehe 21 Septemba 2022 jambo ambalo sio sahihi na hakuna muongozo wala maelekezo hayo,naomba mpuuze jambo hili kwanza aliyesambaza anatumia nembo ya kampuni moja ambayo kampuni hiyo haijui na haihusiki na tangazo hilo,"amesema.

Mbali na taarifa hiyo Waziri huyo pia amezungumzia kuhusu mageuzi ya elimu nchini,na kusema kuwa serikali inafanya mapitio ya sera ya elimu ya mwaka 2014 pamoja na mapitio ya mitaala ili kuboresha sekta ya elimu.

Amesema kuwa Tanzania Visiwani (Zanzibar) na Tanzania Bara zinafanya kwa pamoja mapitio hayo kwa karibu ili kupata mawazo ya wadau wa elimu na wananchi ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan .

"Rais Samia alitutaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha tuinaboresha elimu hususani kuhakikisha kuwa wanafunzi wengi wanakuwa na elimu ufundi na elimu ujuzi na sisi hatutamuangusha tutatekeleza agizo hilo kwa vitendo,"amesema.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post