UHURU KENYATTA : NITAKABIDHI MAMLAKA KWA RAIS MTEULE WILLIAM RUTO SEPTEMBA 13...LAKINI KIONGOZI WANGU NI BABA RAILA ODINGA


Rais Uhuru Kenyatta ameshikilia kuwa mrithi wake anayependelea bado ni kiongozi wa Azimio Raila Odinga.


Haya yanajiri licha ya uamuzi wa Mahakama ya Juu kuunga mkono kuchaguliwa kwa William Ruto mnamo Jumatatu, Septemba 5.


Kenyatta, akizungumza wakati wa mkutano wa viongozi waliochaguliwa katika muungano wa Azimio katika eneo la Masai Lodge katika Kaunti ya Kajiado leo, alisema kuwa nchi ingeelekezwa katika njia ifaayo Raila angechaguliwa kuwa rais.


“Mlijinyima fursa ya kuleta nchi pamoja, hamjamnyima Raila. Nilijitahidi kumfanyia kampeni,” Uhuru alisema.


Wakati huo huo, rais alithibitisha tena kuwa atakabidhi mamlaka kwa Rais mteule William Ruto mnamo Septemba 13 kwa mujibu wa Katiba.


"Nitakabidhi mamlaka nikitabasamu kwa sababu ni jukumu langu la kikatiba, lakini kiongozi wangu ni Baba [Raila Odinga]," Kenyatta alieleza.


Mkuu huyo wa Nchi anayeondoka alitoa maoni yake kuhusu muungano wa Azimio kumteua Kenneth Marende kama mgombeaji wake wa kiti cha Spika wa Bunge la Kitaifa, akiteuliwa na Farah Maalim kama naibu wake na Kalonzo Musyoka kama Spika wa Seneti, akisaidiwa na Stewart Madzayo.


“Kalonzo Musyoka angekuwa Waziri Mkuu bora zaidi. Ninaamini pia angekuwa mwakilishi mzuri wa ajenda yetu katika Seneti,” alisema Kenyatta.


Wakati huo huo, Uhuru amewataka viongozi waliochaguliwa wa Azimio kuungana akionya kuwa huenda wengine wakashawishika kujiunga na miungano mingine.


"Ikiwa ulichaguliwa kwa tikiti ya Azimio, shikamana na na Azimio usiyumbishwe. Je, utanunuliwa kwa shilingi tano au utasimama na Wakenya zaidi ya milioni 50?," Uhuru aliwauliza viongozi waliochaguliwa.


Kenyatta na Odinga wamehudhuria mkutano huo, pamoja na viongozi wengine wa Azimio Martha Karua na Kalonzo Musyoka.


Kufikia sasa Rais Uhuru Kenyatta hajampongeza hadharani naibu wake William Ruto ambaye alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa mwezi uliopita.


Viongozi hao wawili wamekuwa wakikutana na muungano ya vyama vyao kabla ya kufunguliwa rasmi kwa bunge siku ya Alhamisi. Bw Kenyatta ndiye mwenyekiti wa muungano wa Azimio uliokuwa na Bw Odinga kama mgombeaji wake wa urais.


Pande zote mbili zinapanga mikakati ya namna ya kushinda nafasi za Spika katika mabunge hayo mawili.


Hakuna kundi lolote lililopata wingi wa wazi wa wabunge na maseneta .


Bw Ruto atahitaji idadi ya walio wengi kupitisha miswada muhimu, kuidhinisha wateule wa baraza la mawaziri, makatibu wakuu, mabalozi na makamishna wakuu.

Makabidhiano ya mamlaka

Play video, "‘Nimetoa maagizo yote muhimu kwa makabidhiano ya mamlaka’ - Uhuru Kenyatta", Muda 2,30

‘Nimetoa maagizo yote muhimu kwa makabidhiano ya mamlaka’ - Uhuru Kenyatta


Rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumatatu wiki hii alisisitiza kujitolea kwake kusimamia makabidhiano ya amani ya mamlaka kwa utawala ujao.


Katika hotuba yake iliyopeperushwa kwenye runinga Jumatatu jioni, Uhuru alisema kwa kutii kiapo alichotoa alipochukua madaraka cha kuzingatia sheria na kuheshimu maamuzi ya michakato ya mahakama, ataheshimu uamuzi wa Mahakama ya Juu zaidi wa kuidhinisha uchaguzi wa William Ruto kama Rais mteule.

Heshima kwa rais anayeondoka

Rais mteule William Ruto ameweka wazi maono yake ya Kenya ya kidemokrasia ambayo haina vitisho."Hii inaashiria mwisho wa siasa za udanganyifu, usaliti na ujanja," alisema Jumatatu baada ya mahakama ya juu kuishinisha ushindi wake .


"Tunataka siasa za Kenya za siku zijazo - kila kiongozi lazima ahukumiwe kwa kile anachosema na kile anachosema ndicho anachofanya."Bw Ruto anahisi kuwa yeye na wafuasi wake wakati fulani wamenyanyaswa.


"Tunataka kuwa na nchi inayozingatia utawala wa sheria - mfumo wa haki ya jinai utawekwa kwa ajili ya kupata wahalifu na uhalifu - hautatumika tena kwa sababu za kisiasa ... dhidi ya wale ambao wana maoni kinyume na yetu.


Pia ameshikilia kuwa Bw Kenyatta atatendewa vyema.

"Tutaheshimu rais wetu katika kustaafu kwake ... sisi ni watu wa heshima, sisi sio wadogo na hatuna wivu.Amefanya kazi nzuri na atakuwa na nafasi yake katika historia ya Kenya.


Hakuna mtu anayepaswa kushikilia chochote dhidi ya rais wa Kenya.


"Naye Bw Odinga ataheshimiwa' Ruto alisema

CHANZO - BBC SWAHILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments