TFRA KUTUMIA MAONESHO YA NANENANE KUWAFIKIA WAKULIMA WALIOKO PEMBEZONI

Kaimu Meneja wa TFRA Kanda ya kati Joshua Ng'ondya akizungumza na Waandishi wa habari katika maonesho ya wakulima Nanenane Jijini Dodoma .


Na Dotto Kwilasa,DODOMA

KAIMU Meneja wa Mamlaka  ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA),Kanda ya Kati Joshua Ng'ondya amesema ili kufikia malengo ya kilimo cha kisasa,wanatumia fursa ya  maonesho ya wakulima Nanenane kuelimisha wakulima wa pembezoni matumizi bora  ya mbolea kwa usalama na uhakika wa kuvuna zaidi.


Kaimu Meneja huyo wa TFRA amesema hayo leo Julai 7,2022 Jijini hapa  wakati akizungumza na wandishi wa habari walipotembelea  banda la Mamlaka hiyo katika maonesho ya 28 ya wakulima Kanda ya kati yanayofanyika katika viwanja vya Nanenane eneo la Nzuguni Dodoma.


Ng’ondya ameeleza kuwa pamoja na jukumu kubwa walilo nalo kakika kuelimisha wakulima matumizi bora ya mbolea,baadhi yao bado hawana uelewa sahihi na hivyo kupelekea kushindwa kufikia kilimo cha kisasa jambo linalosababisha uhaba wa chakula.


Kutokana na hali hiyo amesema TFRA imechukua jukumu la kuwashauri wakulima hasa katika maonesho hayo kufanya utambuzi wa aina ya mbolea inayohitajika kulingana na aina ya udongo kwa kuzingatia hali ya hewa na aina ya mazao. 


"Mbolea ni kirutubisho katika mmea,ili kukua mmea huhitaji ili mbolea hivyo sisi kama wadau wakubwa wa kilimo tunamshauri mkulima kutambua aina ya mbolea anayotumia na wakati gani anapaswa atumie,"amesisitiza


Pamoja na hayo amesema kwa kushirikiana na asasi za ndani na nje ya nchi zinazoshughulikia mbolea wamekuwa wakitoa elimu kwa wakulima nchini ili kuhakikisha mbolea bora  inamfikia mkulima katiba ubora unaotakiwa na kwa bei himilivu.


Amesema wakulima wanapaswa kulima kilimo biashara na kuachana na kilimo cha mazoea hali itakayowapa nafasi ya kuzalisha kwa tija bila hasara .

Kwa umuhimu huo Ng’ondya ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wakulima kwenda katika ofisi za Watendaji wa mtaa au Kijiji ili waweze kusajiliwa kwajili ya kupata mbolea ya ruzuku huku akitaja faida za kutumia mbolea zinazodhibitiwa na TFRA kuwa ni bora na humfanya mkulima kupata tija iliyokusudiwa.


"Kuna faida kubwa iwapo mkulima atatumia mbolea ziilizosajiliwa na TFRA,mtu yoyote haruhusiwi kufanya biashara ya mbolea bila kuwa na leseni, ili kumruhusu mfanyabiashara kuuza mbolea TFRA imeanzisha mfumo wa kidigitali wa usajili wa wafanyabiashara wa mbolea utakao muwezesha mfanyabiashara yeyote kuingia katika mfumo akiwa nyumbani au mahali popote,"amefafanua

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post