MKENDA AZINDUA TIMU YA UTAFITI WA UFUATILIAJI WAHITIMU MAFUNZO YA UFUNDI VYUO VYA VETA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda 

Na Dotto Kwilasa, DODOMA
 

SERIKALI imeunda timu ya watu watano kwa ajili ya kufanya Utafiti wa ufuatiliaji wa wahitimu wa mafunzo ya ufundi kutoka vyuo vya VETA nchini itakayo ongozwa na Dkt. Hamisi  Mwinyimvua ambaye ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).

Wajumbe wangine  ni pamoja na Prof. Deograsias Mushi ambaye ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Dkt. John Chegere Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Dkt. Claude Maeda Mhadhiri kukota Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Dkt. Ibrahim Kadigi Mhadhiri kukota Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Akitangaza timu hiyo ya Wataalamu hao leo tarehe 16 Agosti 2022 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa tafiti hizo zitalenga Kutathmini athari chanya au hasi za muda mrefu za programu mbalimbali za elimu; Kuboresha mitaala na mazingira ya elimu na mafunzo. 

Mkenda ametaja faida nyingine kuwa zitalenga kujua vikwazo wanavyopambana navyo wahitimu wanapoenda kwenye soko la ajira ili kuboresha na kujua kama elimu au ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira au mahali pa kazi unaendana na elimu au mafunzo yanayotolewa na vyuo husika. 

Amesema malengo hayo yanaonyesha kuwa tafiti za ufuatiliaji zinatoa taarifa muhimu kwa wadau wanaohusika na Utoaji wa Elimu na Mafunzo,kuandaa Sera ya Elimu na Mafunzo,kuandaa Mitaala ya Elimu na Mafunzo ili kuhakikisha wale wote wanaohitaji elimu na mafunzo au ujuzi wa aina fulani wanapata fursa hiyo.

"Malengo haya yanaonyesha ajira na uandaaji wa sera za ajira,kuandaa Sera na Miongozo ya ajira ili kuhakikisha wataalamu wa aina mbalimbali wanaohitajika wanakuwepo ili kutoathiri uwekezaji na ukuaji wa uchumi pamoja na ufanyaji maamuzi ya kifamilia au binafsi, kuhusu aina gani ya elimu au mafunzo ya ujuzi mtoto au mtu asomee ili kukubalika kwenye soko la ajira au kuanzisha biashara binafsi,"amesema.

Waziri Mkenda pia amesema kuwa kwa sababu ya msukumo mkubwa uliowekwa kwenye ujuzi wadau wote wa elimu nchini wanapewa fursa ili waweze kutoa ushirikiano kwa kutoa maoni yao ili kuboresha elimu ujuzi.

Waziri Mkenda amesema kwa Sasa soko la Vyuo vya ufundi liko juu na kufafanua kuwa  wahitimu wa mafunzo ya VETA wameongezeka kutoka 179,930 mwaka 2016 hadi 295,446 mwaka 2020, na kwamba  utafiti wa mwisho wa aina hii ulifanyika mwaka 2018 kwa waajiriwa wa 2010 – 2015.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Fransis Michael amesema kuwa timu hiyo ina kazi kubwa kuhakikisha kuwa inapokea maoni kutoka maeneo mbalimbali ili kuakisi uwajibikaji na ufanisi wa elimu ujuzi.

Amesema kuwa lengo kubwa katika ukusanyaji huo wa maoni ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapomaliza elimu ujuzi waweze kuajirika kirahisi katika maeneo mbalimbali waliyosomea.

Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ambaye ni kiongozi wa timu hiyo Dkt. Hamisi H. Mwinyimvua amesema kuwa utafiti wa aina ya ufuatiliaji unaweza kufanyika kujua walipo wahitimu wa kada au ujuzi fulani  (graduates) au wahitimu kutoka chuo fulani (alumni). 

Ameongeza kuwa lengo la ufuatiliaji linaweza kuwa kujua ajira/shughuli wanayofanya baada ya kuhitimu, jinsi wanavyotumia ujuzi walioupata na changamoto wanazopambana nazo. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post