IJA YATOA MAFUNZO KWA MAKATIBU MUHTASI

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akisisitiza jambo alipokuwa anafungua mafunzo ya siku tano kwa Makatibu Muhtasi 56 yaliyoanza kufanyika.
Sehemu ya Makatibu Muhtasi wanaoshiriki katika mafunzo ikifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Mkuu wa Chuo.
Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote wa mafunzo.

*******************

Na Rosena Suka, Lushoto

Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama ya Rufaa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto leo tarehe 9 Agosti, 2022 amefungua mafunzo ya siku tano kwa Makatibu Mahsusi wapatao 56 wa Mahakama ya Tanzania yanayohusu Namna Bora ya Uendeshaji wa Ofisi.

 Mafunzo hayo yanayofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 09 Agosti ,2022 mpaka 13 Agosti, 2022 katika ukumbi wa Mafunzo uliopo Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Akifungua mafunzo hayo Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amewataka Makatibu Muhtasi kutoa
huduma bora zinazoendana na uwekezaji katika majengo ya Mahakama nchini. 

 Aliendelea kwa kusema kuwa, Mahakama ya Tanzania iko katika maboresho ambayo yanagusa maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu ya majengo na raslimali watu hivyo mafunzo haya yanalengo la kuwaandaa watumishi hao ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea.

“Hivyo lengo la mafunzo yanayotolewa ni kujaribu kuwajengea uwezo na kubadilisha
fikra za watumishi wa Mahakama ili huduma wanazozitoa mahakamani ziendane na
ubora wa majengo ambayo yanaendelea kuboreshwa,” amesema.

Mhe. Dkt. Kihwelo aliwasihi watumishi hao kuwa waadilifu na wachapakazi ili kuipa
sifa nzuri Mahakama ya Tanzania kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kuichafua
Mahakama kama matumizi ya lugha mbaya. Pia aliwaomba watumishi hao
watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi ni wajibu kushirikiana na kuonyesha
waliochojifunza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya
Tanzania, Bi. Beatrice Patrick amewaambia washiriki hao kuwa Mahakama
imejipanga kuwajengea uwezo watumishi wake katika kada mbalimbali ili kuendana
na maboresho yanayoendelea.

Bi. Beatrice Patrick amesema kundi hilo la washiriki wa mafunzo linajumuisha
Makatibu Muhtasi 56, ambapo 50 wametoka katika Mahakama mbalimbali za
Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi, washiriki sita
wakiwa ni waajiriwa wapya.

Amesema kuwa watumishi hao wanapewa mafunzo hayo kwa lengo la
kuwakumbusha majukumu yao ya kazi za Ukatibu Muhtasi, utunzaji wa

kumbukumbu, usimamizi wa ofisi na mawasiliano ya kiofisi, uzalendo na protokali,
mipango ya Mahakama na uboreshaji, huduma kwa mteja, masuala ya saikolojia na
ushauri, mwelekeo wa Mahakama kwa sasa katika mapinduzi ya viwanda kuelekea
Mahakama Mtandao na matumizi ya TEHAMA.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post