ODINGA ATUA MAHAKAMA KUU KUPINGA URAIS WA RUTO

Mahakama Kuu ya nchini Kenya
Raila Odinga
**

Mgombea wa urais wa Muungano wa Azimio Raila Odinga hatimaye amewasilisha rasmi ombi la kupinga uchaguzi wa William Ruto kuwa rais mteule.


Kesi hiyo iliwasilishwa na mawakili wa Raila walioongozwa na wakili James Orengo katika mahakama ya upeo ya Milimani .


Sheria kuhusu kesi ya kupinga uchaguzi wa Urais 2017 inasema kwamba iwapo kesi itawasilishwa katika siku ya mwisho ya muda uliowekwa kuwasilisha kesi hiyo basi lazima ifanyike kabla ya saa nane mchana katika siku hiyo.


Kulingana na wakili wa Muungano wa Azimio Daniel Maanzo , kikosi cha mawakili wa Muungano wa Azimio tayari kimewasilisha kesi hiyo mtandaoni na kwamba watawasilisha stakhabadhi zinazohitajika mahakamani wakati wowote kufikia sasa.
Wakenya wanasubiri kuona maamuzi yatakayo tolewa na mahakama kuu kama yatafanana na maamuzi ya uchaguzi uliopita, katika hali hiyo Mahakama inatarajia kuweka historia nyingine ya kutoa maamuzi.


''Tumewasilisha kesi hiyo kupitia mtandao huku tukisubiri kuleta stakhabadhi ili mahakama hiyo iweze kuthibitisha ombi hilo''.


''Tuna hadi saa nane lakini naweza kuwahakikishia kwamba kila mtu yuko tayari. Kundi la mawakili linaendelea kukusanya nakala za kesi hiyo na zinatarajiwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa'', alisema Maanzo.


Na kufuatia hatua ya kuwasilisha kesi hiyo mahakamani, Muungano wa Azimio una hadi tarehe 23 Agosti , kukikabidhi chama cha UDA, rais Mteule na tume ya uchaguzi IEBC malalamishi hayo.


IEBC itakuwa na siku nne kuwasilisha majibu yao katika mahakama ya upeo. Hii itafungua njia ya kusikilizwa kwa ombi hilo na majaji wa Mahakama ya upeo siku saba baada ya kuwasilishwa - Jumatatu, Agosti 29.


Majaji wa mahakama ya upeo wakiongozwa na rais na Jaji Mkuu Martha Koome watakuwa na hadi Septemba 4, kutoa uamuzi wao kuhusu ombi hilo.


Kulingana na Kifungu cha 140 cha Katiba ya Kenya (2010), mahakama, kupitia kura ya majaji wengi, inaweza kuunga mkono au kubatilisha uchaguzi wa urais. Iwapo ushindi wa Ruto utaidhinishwa, ataapishwa siku saba baada ya uamuzi huo kutolewa - uamuzi unaopingana utasababisha kurudiwa kwa uchaguzi.

Hadi sasa Tume huru ya Uchaguzi nchini Kenya imemtangaza William Samoei Ruto kama Rais Mteule wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Kenya.

Chanzo  - BBC Swahili

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments