Chui
NDUMISO MONA; ni mwanaume mwamba kabisa wa nchini Afrika Kusini ambaye kwa sasa ni gumzo nchini humo baada ya kupambana na chui na kumuua kwa mikono yake mwenyewe.
Ndumiso alipambana na chui anayedaiwa kutoroka kutoka Hifadhi ya Kitaifa ya Kruger (KNP) huko Afrika Kusini.
Akiwa amesimama kwenye mwinuko wa nyumba yake katika Kijiji cha Matsulu Manispaa ya Mbombela huko Mpumalanga, Ndumiso aliyevalia ovaroli, soksi za kijivu na viatu alisimulia masahibu yake yaliyotokea asubuhi ya Julai 21, mwaka huu.
Ndumiso anasema; “Nilikuwa nikibarizi nje ya duka moja na marafiki zangu tuliposikia kuhusu chui anayezurura karibu na nyumba yangu.
“Akili yangu iliniambia nikimbilie nyumbani. Nilikuwa na wasiwasi na wadogo zangu wawili ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi.
“Nilikimbia na kupita nyumbani kwangu nilipomuona chui. Niligeuka na kushangaa akiunguruma nyuma ya mgongo wangu.
“Tulitazamana machoni. Sote tulisimama kwa takriban dakika mbili tukitazamana.
“Moyo wangu ulikuwa ukipiga sana. Nilimuona akifungua kinywa chake, nikaona meno makali. Alikuwa tayari kuruka. Nilikunja ngumi. Hakukuwa na kurudi nyuma.
“Nilijiambia kwamba mmoja kati yetu lazima afe.”
Ndumiso anasema kuwa, dakika 2 baadaye chui huyo alimrukia, wakaanza kupigana hadi chui akafa.”
Cc; @sifaelpaul