MASHINDANO YA ‘CRDB BANK NGALAWA RACE’ YATAJWA KIVUTIO CHA UTALII ZANZIBAR

Waziri wa Maendeleo ya Jamii wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Riziki Pembe Juma (watatu kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni mbili na nusu (2,500,000/-), Khatib Haji Hamis (wapili kushoto) aliyeibuka mshindi wa jumla katika mashindano ya ‘CRDB Bank Ngalawa Race' yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB katika Tamasha la Kizimkazi, yaliyofanyika leo Agosti 30, 2022 kwenye fukwe za Kizimkazi Mkunguni, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Rajab Yussuf Mkasaba pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa CRDB Insurance Broker LTD, Wilson Mnzava. Picha zote na Othman Michuzi.
---
Kizimkazi, Zanzibar Agosti 30, 2022 – Waziri wa Maendeleo ya Jamii Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma amesema mashindano ya ‘CRDB Bank Ngalawa Race' yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB katika Tamasha la Kizimkazi ni mfano wa michezo ya utamaduni inayotangaza utalii visiwani humo.

Mhe. Riziki ameyasema hayo wakati akifungua mashindano katika hafla iliyofanyika kwenye fukwe za Kizimkazi Mkunguni ambapo mamia ya watu walijitokeza kushudia mtanange mkali wa washiriki mahiri 20 wa mchezo wa ‘Resi za Ngalawa’ kutoka Kizimkazi Mkunguni na Kizimkazi Dimbani.

“Ni imani yangu ni kuwa mchezo huu utasaidia kuongeza thamani kwa fukwe zetu kwa kutoa burudani kwa watalii wanaotembelea katika visiwa vyetu, na kutoa ajira kwa vijana wetu,” amesema huku akitoa changamoto kwa Wizara za Michezo na Utalii kushirikiana na Benki hiyo kuendeleza mchezo huo.

Aidha, aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia jitihada za Serikali katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii na kuwaletea wananchi maendeleo. “Niwapongeze kwa namna ambavyo mnajitoa kusaidia jamii. Ufadhili wenu katika miradi ya maendeleo hapa Kizimkazi unaonyesha kiu mliyonayo katika kuboresha maisha ya Watanzania.”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa alisema Benki hiyo imeamua kuwekeza katika mchezo huo wa ‘Resi za Ngalawa’ kwa kuwa ni moja ya michezo ya asili hapa nchini ambayo ikitangazwa vizuri inaweza kutangaza utamaduni wa Wazanzibari na kuvutia watalii kuja kutembelea nchini.

“Rais wetu Mama Samia amefanya jitihada kubwa katika kutangaza vivutio vya utalii nchini kupitia filamu ya ‘Royal Tour’, tukiwa Benki kiongozi na ya kizalendo nchini tumeona ni vyema kuunga mkono jitihada hizi kupitia mashindano haya ambayo asili yake ni katika visiwa hivi vya Zanzibari,” amebainisha.
Akielezea lengo jingine la kuandaa mashindano hayo kwa mwaka wa pili mfululizo kupitia Tamasha la Kizimkazi, Tully alisema Benki ya CRDB pia imedhamiria kuutumia mchezo huo wa Resi za Ngalawa kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuufanya mchezo kuwa wa kibiashara kama ilivyo michezo mingine.

“Katika kutekeleza azma hii, mwaka huu tumekabidhi vifaa vipya kwa washiriki wote 20 vyenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 50 ikiwamo ngalawa za kisasa na maboya ya uokoaji. Hii imeongeza hamasa kubwa sana kwa washiriki ambapo mashindano ya mwaka huu yamekuwa na ushindani mkubwa.”
Washiriki hao 20 walishindana katika resi za maili 2 kwa mizunguko miwili ambapo Khatib Haji Hamis mkaazi wa Kizimkazi Mkunguni aliibuka mshindi wa kwanza na kuondoka na zawadi ya shilingi milioni 2.5 na boti ya uvuvi kwa ajili ya kikundi kutoka kijiji anachotoka.


Mshindi wa pili alikuwa Juma Ramadhani Haji kutoka kijiji cha Kizimkazi Mkunguni ambaye aliondoka na kitita cha shilingi milioni 1, na watatu alikuwa Muhammad Ambar Mpate kutoka kijiji cha Kizimkazi Mkunguni ambaye aliibuka na zawadi ya shilingi laki 7, na mshindi wan ne alikuwa Daudi Wajihi Zahor mkazi wa Kizimkazi Dimbani ambaye alijishindia shilingi laki 5.


Mbali na mchezo wa wa “Resi za Ngalawa”, Benki ya CRDB pia imetumia zaidi ya shilingi milioni 65 kudhamini michezo mingine katika Tamasha la Kizimkazi ikiwamo; mpira wa miguu, mpira wa pete, nage, mbio za baiskeli, bao, kukuna nazi, kuvuta kamba, na uchoraji.Aidha, Benki hiyo pia imejenga maabara ya kisasa ya sayansi iliyokamilika pamoja na vifaa vyake katika Skuli ya Kizimkazi yenye thamani ya shilingi milioni 50. Maabara hiyo inalenga kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sanyansi.

Tamasha la Kizimkazi linatarajiwa kufikia tamati siku ya jumamosi ya tarehe 3 Agosti 2022 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan. Miradi mbalimbali ya maendeleo inatarajiwa kukabidhiwa siku hiyo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Riziki Pembe Juma akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mashindano ya ‘CRDB Bank Ngalawa Race' yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB katika Tamasha la Kizimkazi, yaliyofanyika leo Agosti 30, 2022 kwenye fukwe za Kizimkazi Mkunguni, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa, akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mashindano ya ‘CRDB Bank Ngalawa Race' yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB katika Tamasha la Kizimkazi, yaliyofanyika leo Agosti 30, 2022 kwenye fukwe za Kizimkazi Mkunguni, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Mshindi wa kwanza wa CRDB Ngalawa Race, Khatib Haji Hamis akiwa juu ya boti iliyokabidhiwa zawadi kwa kijiji chake cha Kizimkazi Mkunguni kwa ajili ya kuchochea maendeleo. Boti hiyo ina thamani ya shilingi milioni 25.
Sehemu ya Ngalawa zilizoshiriki katika mashindano ya ‘CRDB Bank Ngalawa Race' yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB katika Tamasha la Kizimkazi, yaliyofanyika leo Agosti 30, 2022 kwenye fukwe za Kizimkazi Mkunguni, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Elias Barnabas maarufu kama Barnaba akitoa burudani wakati wa mashindano ya ‘CRDB Bank Ngalawa Race' yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB katika Tamasha la Kizimkazi, yaliyofanyika leo Agosti 30, 2022 kwenye fukwe za Kizimkazi Mkunguni, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Mgeni Rasmi akiwa katika picha za pamoja na washiriki wa Timu zote mbili (Kizimkazi Dimbani na Kizimkazi Mkunguni) wakati wa mashindano ya ‘CRDB Bank Ngalawa Race' yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB katika Tamasha la Kizimkazi, yaliyofanyika leo Agosti 30, 2022 kwenye fukwe za Kizimkazi Mkunguni, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Sehemu ya wananchi wakiendelea kufurahia burudani mbalimbali katika mashindano ya ‘CRDB Bank Ngalawa Race' yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB katika Tamasha la Kizimkazi, yaliyofanyika leo Agosti 30, 2022 kwenye fukwe za Kizimkazi Mkunguni, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post