WATALII 35 KUTOKA ISRAEL WATUA ROMBO

  

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akiongea na wananchi katika Kijiji cha Simbalo,Kata ya KatangaraMlele,Rombo.

Na Mathias Canal, KILIMANJARO 

WADAU wa maendeleo kutoka nchini Israel wanaojulikana kama Upendo Group wamewasili hapa nchini,mkoani Kilimanjaro katika Wilaya ya Rombo kwa wiki mbili kuanzia tarehe 26 Julai 2022 mpaka  Agosti 6,2022 kwa ajili kufanya utalii na kuunga mkono maendeleo.

Pamoja na kufanya utalii lakini kikundi hicho kitakarabati madarasa mawili ya shule ya msingi Simbalo, ujenzi wa jiko la shule, kuweka mtandao wa umwagiliaji (Drip Irrigation) kwenye kilimo cha mbogamboga kwa ajili ya wanafunzi shuleni hapo.

Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Simbalo, Kata ya KatangaraMlele mara baada ya kuwapokea watalii hao, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema  watalii hao 35 wa kikundi cha Upendo Group wamekusudia kuunga mkono juhudi za serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kufanya shughuli za jamii ikiwemo kuboresha miundombinu ya madarasa.

Pamoja na hayo amewashukuru watalii hao kutoka Israel ambao wamejitolea kuendeleza juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya elimu.

"Rais Samia Sulu Hassan ametoa fedha nyingi kwenye Wizara ya Elimu kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo ikiwemo fedha za UVICO 19 zilizofanya kazi nzuri kujenga madarasa 15,000 kwa shule za msingi pamoja na shule shikizi ambapo katika Wilaya ya Rombo ilipata shule shikizi moja na madarasa 44 huku kwa upande wa shule za sekondari kupitia mpango huo yamejengwa zaidi ya madarasa 20,000,"amesema.

Waziri Mkenda amesema kuwa Rais Samia ametilia mkazo zaidi katika kuimarisha sekta ya elimu ambapo pamoja na juhudi zote za serikali lakini serikali haifungi milango kwa watu wenye uwezo wa kuunga mkono jitihada za serikali.

"Serikali sasa inatoa elimu bila ada haijasema wananchi kwa hiari yao wasijitolee kuendeleza sekta ya elimu, kwa wale wenye uwezo wa kujenga madarasa, kununua madawati na mengineyo ni vizuri wenye uwezo wa kuchangia juhudi za serikali waendelee kufanya hivyo" Amekaririwa Waziri Mkenda

Waziri Mkenda amesema kuwa aibu ya changamoto ya vyoo shuleni ni lazima kuimaliza.

 "Waziri wa TAMISEMI Mhe Innocent Bashungwa amesema ataanza kampeni ya ujenzi wa vyoo na mimi namuunga mkono na wananchi tumuunge mkono ili kuboresha mazingira ya shule ili yawe ni mahali pazuri kwa wanafunzi ili waweze kupenda kusoma" amesema Waziri Mkenda

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments