WAGOJWA WA MOYO 50 WATIBIWA HOSPITALI YA KANDA CHATO

Wananchi wakiendelea kupata matibabu bure kwenye hospitali ya rufaa ya kanda Chato

***


Na Daniel Limbe, Chato

KUELEKEA mwaka mmoja wa huduma za afya kwenye hospitali ya rufaa ya kanda Chato, zaidi ya wagonjwa wa moyo 50 wamepatiwa matibabu ya kibingwa hali iliyosaidia kunusuru maisha yao.

Mbali na hao,takribani wagonjwa 10500 wamepatiwa huduma za matibabu ya magonjwa mbali mbali ikiwemo, afya ya mama na mtoto,uzazi,dharula na zile za wagonjwa mahututi.

Akisoma risala kwenye ufunguzi wa wiki ya huduma kwa wateja inayolenga kutoa matibabu ya kawaida na yale ya kibingwa bure kwa wagonjwa mbali mbali,kaimu mganga mkuu wa hosptali hiyo, Dk. Osward Lyapa, amesema uwepo wa hospitali hiyo imekuwa ni faraja kubwa sana kwa jamii baada ya huduma za magonjwa makubwa kupatikana umbari mfupi ikilinganishwa na iwapo wagonjwa wangepelekwa hospitali ya Jakaya Kikwete jijini Dar es salaam.

Awali mtaalamu wa huduma za mionzi kwenye hospitali hiyo, Magesa Mokiri, amedai mpaka sasa wagonjwa wa moyo 50 wamepokelewa na kupatiwa huduma za kibingwa na kwamba jamii imeanza kutambua thamani ya uwepo wa hospitali hiyo.

Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuiomba serikali kutatua changamoto ya uhaba wa wataalamu wa tasnia ya mionzi kutokana na waliopo sasa kuwa watatu pekee licha ya mahitaji kuwa ni watumishi 8.

Mbali na kuipongeza serikali Mbunge wa jimbo la Chato, Medard Kalemani, amewataka wananchi kuilinda na kuitunza miundombinu ya hospitali hiyo ili idumu kwa lengo la kuwahudumia watanzania wote wenye uhitaji wa matibabu ya kawaida na yale ya kibingwa.

Kadhalika ameiomba serikali kusaidia upatikanaji wa gari la wagonjwa, utawala pamoja na lile la kukusanyia damu salama hatua itakayosaidia upatikanaji wa huduma bora zaidi kwa jamii.

Mkuu wa wilaya hiyo, Martha Mkupasi,ambaye pia alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja, ametumia jukwaa hilo kuwahamasisha wazazi kusomesha watoto wao masomo ya sayansi ili baadaye wanufaike na ajira za afya ambazo ni muhimu sana kwa jamii yoyote duniani.

"Wazazi nawashauri sana msomeshe watoto wenu masomo ya sayansi...hebu fikiri utajisikiaje unapokuja hapa kutibiwa halafu ukatibiwa na mwanao"..? alihoji Mkupasi.

Huduma za afya bure zimeanza kutolewa Julai 27 na zitarajiwa kuhitimishwa Julai 30 mwaka huu kwenye viunga vya hospitali hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments