MTAKA KUONGOZA WANANCHI KUWASHA MWENGE KUENZI MASHUJAA

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya kitaifa ya Sikukuu ya mashujaa yatakayofanyika Julai 25,2022 Jijini Dodoma.


Na Dotto Kwilasa, DODOMA

KUELEKEA kumbukumbu za mashujaa ,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Ofisi ya maadhimisho ya kitaifa wataongoza wananchi mkoani hapa kwenye zoezi la uwashaji wa mwenge kwenye mnara wa kumbukumbu ya mashujaa usiku wa kuamkia kilele cha maadhimisho hayo Julai 25,2022.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema hayo leo Julai 21,2022 Jijini hapa wakati akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kukagua maandalizi ya sherehe hizo na kueleza kuwa tayari mandalizi yote yamekamilika.


Amefafanua kuwa zoezi la uwashaji wa mwenge ni ishara ya kuenzi na kukumbuka mchango wa mashujaa hao na kwamba Julai 24,2022 saa sita usiku atawaongoza wananchi kushuhudia zoezi la uwashaji wa mwenge huo kisha kuuzima saa sita usiku wa tarehe Juali 25,2022 baada ya kumalizika kwa kilele cha maadhimisho hayo.


Kwa umuhimu wa tukio hilo, Mtaka amesema Ofisi yake itafanya tukio hilo kuwa la aina yake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha changamoto zote zikiwemo za hali ya mnara na mazingira yake zinakuwa sawa ili kuhakikisha eneo hilo linakuwa hai kama maeneo mengine duniani.


Kutokana na hayo Mtaka amesema,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ,Ofisi ya Jiji na Ofisi ya maadhimisho ya kitaifa watakaa pamoja kuona namna ya kutunza eneo hilo na kulifanya liwe la kisasa ikiwa ni pamoja na kuboresha hali ya mazingira yake.


"Niwahakikishie kuwa mwakani changamoto zote hazitakuwepo tena tutaweka mpango mzuri kwa kulenga kuwa na eneo la mashujaa ambapo wakati wote watu watahitaji kuona kuja kwenye hili eneo, tutaona ubunifu gani zinahitajika kufanyika hapa ili kupachangamsha,"amesema


Sikukuu ya mashujaa huadhimishwa ifikapo Julai 25 ya kila mwaka ambapo umuhimu wake kwa Tanzania ni tofauti na mataifa mengine kwani watanzania wako huru zaidi kwenda kokote wanakotaka na hata kuishi ama kufanya kazi au biashara bila ya bughudha yeyote kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za nchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments