WATU SITA WA FAMILIA MOJA WAUAWA KIKATILI ..ABAKIZWA MTOTO MDOGO TU

Abak
Eneo la tukio Kitongoji cha Kakonkwe kijiji cha Kiganza Halmashauri ya wilaya Kigoma

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

WATU sita wa wa familia moja akiwemo bibi kizee mwenye umri wa miaka 70 aliyefahamika kwa jina la Tilifera Toyi (70) wameuawa kwa kukatwa katwa na vitu vyenye ncha kali kichwani na kwenye maeneo mbalimbali ya miili yao.

Kaimu Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Menrad Sindano akitoa taarifa kwa waandishi wa habari amesema tukio hilo limeikumba familia hiyo ya watu wanane kutoka Kitongoji cha Kakonkwe kijiji cha Kiganza Halmashauri ya wilaya Kigoma na hakuna mtu aliyekamatwa hadi sasa kuhusiana na tukio hilo.

Kaimu Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma amewataja wengine waliouawa kuwa ni Januari Mussa na (35) na Joel Mussa (40) ambao ni ndugu wa tumbo moja sambamba na Sara Dunia (28) ambaye ni Mke wa Januari.

Pia mauaji hayo yaliwakumba ndugu wengine wa familia hiyo ambao aliwataja kuwa ni pamoja na Christina Lazaro (9) na James Joel (7) huku mtoto James Januari (4) akijeruhiwa na amelazwa hospitali ya mkoa Kigoma Maweni kwa matibabu.

Mkuu wa wilaya Kigoma, Ester Mahawe akizungumza kwa njia ya simu na malunde 1 blog amesema kuwa tukio hilo lililotokea mida ya saa nane usiku wa leo Jumapili Julai 3,2022 kijiji cha Kiganza halmashauri ya wilaya Kigoma ambapo watu wote walikuwa wamelala.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa katika maelezo waliyopata kwa watu mbalimbali wanasema kwamba hakukuwa na purukushani zozote ambazo zimeripotiwa kuonyesha kulikuwa na shida wakati wa tukio hilo.

“Kwa sasa ni vigumu kusema sababu ya tatizo hilo kwa sababu hakuna mtu yeyote ambaye amekamatwa kuhusiana na tukio hilo na vyombo vya ulinzi na usalama vimeanza uchunguzi kuhusiana na tukio hilo hivyo taarifa zaidi zitatolewa kadri tunavyofanya uchunguzi,”amesema Mkuu huyo wa wilaya.

Katika tukio hilo wauaji hawakumgusa wala kumjeruhi mtoto Agness Januari mwenye umri wa miezi mitatu ambaye kwa sasa amehifadhiwa kwa ajili ya usalama wake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post