MAKAMBA ATAKA WAKANDARASI WAZAWA KUONESHA WELEDI

 

Waziri wa Nishati January Makamba akitoa maelekezo kwa wakandarasi wanaotekelezwa mradi mkubwa wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) kuja Chongoleani Tanga jana katika kijiji cha Sojo, kata ya Ugusule, wilayani Nzega Mkoani Tabora ambapo kinajengwa kiwanda cha kuandaa mabomba ya kusafirisha mafuta hayo kwenda jijini Tanga

Na Mwandishi wetu, Tabora

WAKANDARASI wazawa waliopewa kazi katika mradi mkubwa wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda kuja Chongoleani (Tanga) wametakiwa kufanya kazi kwa weledi ili serikali iendelee kuwaamini na kuwapa kazi nyingine.

Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Nishati January Makamba alipofanya ziara maalumu kutembelea eneo kinapojengwa kiwanda kikubwa cha kutengeneza mabomba yatakayotumika kusafirisha mafuta ghafi ya mradi huo.

Alisema kiwanda hicho kinachojengwa katika Kijiji cha Sojo, Kata ya Igusule, wilayani Nzega Mkoani hapa kinatakiwa kukamilika haraka kwa ubora na weledi unaotakiwa ili kazi ianze kutokana na umuhimu wake kwa uchumi wa taifa.

Alibainisha kuwa makampuni ya ndani yanaposhiriki katika miradi mikubwa kama hiyo wanapata uzoefu na nchi inapata manufaa lakini wanapofanya vibaya au kuchelewesha kazi wanakwamisha juhudi za serikali na kutokuaminika.

 ‘Miradi huu una manufaa makubwa kwa serikali, hivyo wakandarasi wa ndani wanaposhirikishwa wanapaswa kufanya kazi kwa weledi na viwango ili iwe rahisi kupata kazi nyingine zinazotekelezwa hapa nchini’, alisema.

Waziri Makamba aliongeza kuwa matarajio ya serikali ni mradi huo kuanza kazi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu hivyo akaagiza kila mkandarasi aliyepewa kazi katika mradi huo kutimiza wajibu wake ipasavyo.

Alizitaka kampuni zote kushirikiana ili kuharakisha utekelezaji wake, alitaja baadhi ya kampuni hizo kuwa ni Milembe Construction Company Ltd (ya wazawa), ECOP (East African Crude Oil Pipe line) na ISOAF ambao wamepewa kazi ya kutengeneza kiwanda hicho.

Mbunge wa Jimbo la Bukene Seleman Zedi ambapo mradi huo upo, aliishukuru serikali kwa kuleta mradi huo katika kijiji hicho na kuwapelekea umeme wa uhakika katika eneo hilo, sasa wananchi wameanza kunufaika kwa kupata ajira.

Aliongeza kuwa serikali pia imewapatia kiasi cha sh mil 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika kata hiyo ili kuboresha huduma za afya kutokana na muingiliano wa watu wengi aidha alisema halmashauri pia inatarajia kupata tozo ya huduma kiasi cha sh bil 1.8 kutokana na mradi huo.

Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alisisitiza kuwa dhamira yao ni kuona mradi huo ukiwanufaisha wakazi wa Mkoa huo katika nyanja zote ikiwemo ajira, kupata fursa ya kutoa huduma za chakula, ulinzi na mengineyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments