MBUNGE EZRA AREJESHA TABASAMU KWA WANAFUNZI AJALI YA MOTO, WADAU WAMUUNGA MKONO

Wakwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo Mh. Kemilembe Lwota akiwa ameshika godoro ili kukabidhi kwa wanafunzi na Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi Mhandisi Ezra Chiwelesa watatu kushoto
Wanafunzi wa shule ya sekondari Mubaba iliyopo kata ya Kiniha Wilayani Biharamulo wakiwa wamepokea msaada wa magodoro
Bweni lililoteketea kwa Moto katika shule ya sekondari Mubaba iliyopo kata ya Kiniha Wilayani Biharamulo Mkoani Kagera
Bweni lililoteketea kwa Moto katika shule ya sekondari Mubaba iliyopo kata ya Kiniha Wilayani Biharamulo Mkoani Kagera



Na Mbuke Shilagi Kagera.

Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi Mhandisi Ezra Chiwelesa arejesha tabasamu kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Mubaba iliyopo kata ya Kiniha Wilayani Biharamulo baada ya ajali ya moto ya bweni lililoteketea na kusababisha hasara kubwa mnamo Julai 17,2022 majira ya saa 12  jioni.

Akizungumza mara baada ya kufika eneo la tukio Mbunge huyo amesikitishwa na hali aliyoikuta shuleni hapo na kuitaka jamii kwa kushirikiana na Serikali kulichukulia suala hilo kama dharula na kutoa msaada kwa haraka.


Aidha katika kuhakikisha anatoa pole na faraja kwa wanafunzi , Mbunge Ezra ametoa magodoro 50 huku akiungwa mkono na mgodi wa Stamico waliotoa magodoro 50 pamoja na kampeini ya Alsamood ya wilayani Biharamulo waliotoa mashuka Zaidi ya 280 kwa wanafunzi hao.

Pia amewaomba wadau mbalimbali kuendelea kutoa msaada ili kuweza kuwasaidia wanafunzi hao huku akieleza kuwa kamati ya ulinzi na usalama imemteua katibu tawala wa Wilaya hiyo kuwa Mratibu na mpokeaji wa misaada hiyo.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya Biharamulo Mh. Kemilembe Lwota amesema kutokana na dharula iliyopo tayari ameshatoa maagizo kuanza kwa ujenzi wa bweni hilo mara Moja na kusisitiza kuwa kufikia jumamosi ya Julai 23 Mwaka huu wanafunzi wawe wamerejea kwenye bweni hilo.

Mh. Kemilembe amewasihi wanafunzi kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki huku serikali ikishughulikia jambo lao na kuwataka Wazazi kuwa na amani kuwa watoto wao wako salama huku akieleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama bado vinafanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post