MTOTO ALIYEJERUHIWA NDUGU ZAKE SITA WAKIUAWA KIKATILI KIGOMA AFARIKI

Makaburi ya pamoja ya watu sita wa familia moja ambao waliuawa kwa kukatwa katwa na vitu vyenye ncha kali waliozikwa kwenye kijiji cha Kiganza Jumapili jioni


Na Fadhili AbdallahKigoma


Mtoto James Januari (4) aliyejeruhiwa katika tukio la mauaji ya watu sita wa familia moja yaliyotokea kwenye kijiji cha Kiganza Halmashauri ya wilaya Kigoma amefariki usiku wa kuamkia leo.


Mganga Mfawidhi wa hospitali ya mkoa Kigoma Maweni,Dk.Stanley Binagi amethibitisha kifo cha mtoto huyo kilichotokea kwenye hospitali ya mkoa Morogoro akiwa njiani kupelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.


Dk.Binagi alisema kuwa awali Marehemu James alikuwa amelazwa katika Hospitali ya mkoa Kigoma Maweni chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa ajili ya uangalizi zaidi baada ya kujeruhiwa vibaya kwenye tukio hilo.

Mganga huyo Mfawidhi wa hospitali ya mkoa alisema kuwa marehemu alikuwa ameathirika mgongoni na kwenye fuvu la kichwa na kufanya sehemu ya mwili wake kutokuwa na mawasiliano.


Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa wilaya Kigoma,Ester Mahawe alisema kuwa walifanikiwa kumpa rufaa mtoto huyo kwenda Muhimbili na aliondoka Kigoma Jumatatu jioni kwa gari akiwa na ndugu na wahudumu wa afya lakini alipofika Morogoro hali yake ilibadilika na kupelekwa hospitali ya mkoa Morogoro kwa msaada ambapo alifariki baadaye.


Kufuatia kifo hicho Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa amewasiliana na viongozi wa kata na kijiji cha Kiganza kutoa taarifa kwa familia ya mtoto huyo na kuandaa taratibu za mazishi ambapo mazishi yanaweza kufanyika kesho baada ya mwili kutarajiwa kufika leo jioni.

Kifo cha mtoto Januari kinafanya idadi ya watu waliokufa kwenye tukio hilo kufikia saba ambapo mtoto mwenye umri wa miezi mitatu alinusurika akiwa hajadhurika na kwa sasa amehifadhiwa kwa ajili ya matunzo na usalama wake.

Jeshi la polisi chini ya usimamizi wa Kamishna wa operesheni na mafunzo, Liberatus Sabas limeanza uchunguzi wa tukio hilo huku Kamishna huyo wa polisi akiahidi kuwatia mbaroni wahusika katika kipindi kifupi kijacho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments