BASHUNGWA AWASIMAMISHA KAZI WATUMISHI WATANO MANYARA..."KWANINI TUBEMBELEZANE..SUBIRI MUONE'

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa ameagiza kusimamishwa kazi na kuhojiwa na Taasisi Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) watumishi watano kutokana kuisababishia hasara Halmashauri ya Wilaya Kiteto mkoani Manyara.


Waziri Bashungwa amechukua hatua hiyo wakati wa ziara yake Wilayani hapo tarehe 28.07.2022.

Watumishi hao ni aliyekuwa Mweka Hazina Ndugu Nassoro P. Mkwanda na Mhasibu wa Mapato Ndugu Christopher G. Mwigani, Kaimu Mwanasheria wa Halmashauri Ndugu Joseph J. Hoza, Kaimu Mweka Hazina Ndugu Hadija Boffu pamoja na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi Nakaji Mollel.

Kati ya hao Ndugu Nassoro Mkwanda aliyehamishiwa Mafinga Mji, Khadija Bofu aliyehamishiwa Songea Manispaa na Christopher Mwigani ambaye amestaafu wote wanatuhumiwa kuhamisha fedha na kuweka kwenye akaunti ya amana isiyo na vifungu vya matumuzi na wanatakiwa kurejeshwa kwenye Halmashauri hiyi kujibu tuhuma hizo.

Pia Kaimu Mkuu wa kitengo cha manunuzi Nakaji Melateki Mollel ambaye aliidhinisha Sh milioni 191.9 kwa ajili ya kununua vifaa vya ujenzi bila kufauta taratibu sambamba na Sh milioni 235.5 alizolipa mkandarasi wa kuchimbia visima bila kuzifanyiwa tathimini na Khalfan Hinga aliyetoa kazi hiyo bila kufanyika tathimini.

Amekemea tabia ya kuwahamisha watumishi waliofanya vibaya kwenye halmashauri na kusisitiza kuwa atawafuata popote walipo.

Bashungwa ametoa maagizo hayo wakati wa kuhitimisha ziara yake wilayani Kiteto mkoani Manyara kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) 2019/20 na ile ya mwaka 2020/21 imeelekeza watumishi hao kuchukuliwa hatua kutokana na makosa hayo.

" Nilishakataza tabia ya mtumishi anafanya madudu halmashauri A na anahamishiwa halmashauri B, mtu alifanya madudu na kuhamisha tutamfuata huko huko. Maelekezo ya CAG lazima yatekelezwe kwa mapana yake hawa watumishi wanatakiwa kuwa Takukuru wanachunguzwa. Hawa watumishi wafutuliwe na sheria ichukuwe mkondo wake."

" Kwenye hili hatutanii, hiyo aliyeko Mafinga na wa Songwe waje wajibu tuhuma zao na huyo Hoza aliyekwenda Dodoma huko huko Sheria ifuate mkondo wake. Hii tabia ya kuhamisha hamisha mtu anatenda madhambi anakwenda kwenye halmashauri anafuatwa huko huko, sheria zipo maabusu zipo, sasa kwa nini tubembelezane?

" Nimepewa kazi ya kusimamia, subiri muone, nitakwenda kwenye kila Halmashauri na hizi taarifa haziozi ukifanya mkosa halmashauri A ukaenda B nitakufuata huko huko, haiwezi kuwa kwenye utumishi wa umma na si msafi."

Pia Bashungwa alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere kuhakikisha wanaodaiwa kiasi cha Sh milioni 224.5 ambazo zilioneshwa kukusanya lakini hazikufika Benki kuwa wamerudishwa sambamba na kupiga mnada mali za mtumishi ambaye hakupeleka fedha benki ili kufikia fedha za Serikali.

Aidha, Bashungwa alisema kuna haja ya kuhoji Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri pale panapokuwa na ubadhilifu wa fedha kwa sababu ndio wanaohusika usimamizi.

Alisema ni lazima wakuu wa mikoa na wilaya kote nchini kusimamia ipasavyo Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa ubainisha na kuchukua hatua kwa wakati.

" Tusisubiri na kukaa nyuma mpaka CAG anakuja kutukagua na kufanya chambuzi ndio tuchukue hatua, Tunapaswa kuchukua hatua kwa wakati. Katibu Tawala wa Mkoa ndio Mtendaji Mkuu na sheria imeampa mamlaka ya kuchukua hatua za kinidhamu kwa mtumishi yeyote ambaye yuko kwenye Mkoa ambaye anapenda tofauti na sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma."

Pia ashungwa amekema tabia ya hamashauri kushindwa kuhuisha leseni za biashara kwa muda jambo ambalo linakosesha mapato.

Taarifa ya CAG imeonesha halmashauri hiyo ilikosa mapato takribani Sh milioni 177.3 ambazo halmashauri ingezipata endapo wangehuisha leseni za biashara kwa mujibu wa taratibu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments