MBARONI KWA MADAI YA KUMUUA HOUSE GIRL WAKE KISHA KUFICHA MWILI KWENYE STOO YA VIFAA VYA UJENZI DAR


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limemkamata Selemani Haruna maarufu Kwata (24), kwa tuhuma za kumuua Editha Charles (22), Binti wa kazi za ndani na kuuficha mwili huo katika stoo ya vifaa vya ujenzi katika nyumba ya Agatha Stanslaus Jijini Dar es Salaam.


Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Jumanne Muliro amesema kuwa uchunguzi wa awali umeonesha mnamo Julai 06, 2022 majira ya asubuhi mtuhumiwa huyo alifika kwenye nyumba aliyokuwa anayoishi Binti huyo wa kazi akijifanya fundi wa umeme na kwamba alitakiwa kuweka Balbu.


Kamanda Muliro amesema kuwa baada ya kuingia alimshambulia kwa kitu chenye ncha kali Binti huyo na kumuua halafu akavunja chumba cha mwenye nyumba na kuiba Tsh 1,800,000 na kutoweka.

“Polisi kwa Kutumia Watalaamu wake wa uchunguzi wa kisayansi na vyanzo vingine vya kiuchunguzi walibaini Mtuhumiwa huyo kuwa aliingia kwenye nyumba hiyo na kukaa kwa masaa kadhaa na kutoka" amesema Kamanda Muliro


Ameongeza kuwa baada ya kumkamata na kumhoji kwa kina alikiri kumuua Binti huyo, kuvunja mlango wa chumba na kuiba pesa Tsh 1,800,000 na mwili wa marehemu aliuficha kwenye stoo ya nyumba hiyo huku akiwa ameufunika na vifaa mbalimbali vya ujenzi ili usionekane.

“Alionesha pesa alizoziiba eneo hilo na pesa nyingine alidai mara baada ya tukio siku iliyofuata alinunua simu mpya, viatu vya mpira pea 2, na begi la mgongoni lenye nguo mbalimbali mpya ambavyo navyo vimepatikana" ameelezea Kamanda Muliro


Kamanda Muliro amesema kitendo alichofanya Mtuhumiwa ni cha ukatili uliopitiliza na kuongeza baada ya Uchunguzi kukamilika atafikishwa Mahakamani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post