KIONGOZI WA MWENGE WA UHURU AWEKA JIWE LA MSINGI KITUO CHA MAFUTA CHA KISHUSHU PETROL STATION ISELAMAGAZI


Kituo cha Mafuta Kishushu (Petrol Station) kilichopo Iselamagazi kikiwekewa Jiwe la Msingi na Mwenge wa Uhuru.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022, Sahili Nyanzabara Geraruma, akiweka Jiwe la Msingi katika Kituo cha Mafuta Kishushu (Petrol Station) kilichopo Iselamagazi, (kulia) ni Mkurugenzi wa Kituo hicho Bundala Kishushu.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022, Sahili Nyanzabara Geraruma, akisalimiana na Mkurugenzi wa kituo cha Mafuta Bundala Kishushu.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2022, Sahili Nyanzabara Geraruma, ameweka Jiwe la Msingi katika Kituo cha Mafuta cha Kishushu kilichopo Iselamagazi wilayani Shinyanga.

Iselamagazi ni Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, lakini hapakuwa na Kituo cha Mafuta, ndipo Mwekezaji huyo Bundala Kishushu akaamua kuwekeza kituo hicho na kutatua changamoto hiyo.

Akizungumza kwenye Kituo hicho cha Mafuta Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, amempongeza Mwekezaji huyo kwa kutatua changamoto hiyo ya ukosefu wa mafuta Makao Makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga pamoja na kutoa ajira kwa vijana.

“Nimekagua Mradi huu ni mzuri na Mwekezaji huyu analipa Kodi ya Serikali, isipokuwa kuna tatizo kidogo juu ya wafanyakazi wake hawana mikataba, hivyo anapaswa kuwapa mikataba hata ya muda,”amesema Geraruma.

“Mikataba ni muhimu sana kwa Wafanyakazi wako, mfano siku ukiibiwa pesa hutaweza kumshtaki  kwa sababu anaweza kukataa siyo mfanyakazi wako, na utamkakamtia wapi kwa sababu hukuandikishana naye Mkataba, Mradi mzuri ila wape Mkataba Wafanyakazi wako,”ameongeza.

Naye Mkurugenzi wa Kituo hicho cha Mafuta Bundala Kishushu, amesema amewekeza Kituo cha Mafuta ili kujiinua kiuchumi pamoja na kutatua changamoto ya uhaba wa mafuta eneo hilo la Iselamagazi na kutoa ajira kwa vijana, na ujenzi wake hadi sasa umegharimu Sh. milioni 228.1.

Mwenge wa Uhuru upo Mkoani Shinyanga, ambapo umepokelewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema ukitokea Geita, na umeanza kukimbizwa katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, na umezindua miradi na kuweka Mawe ya Msingi katika Miradi Mitano ya Maendeleo, na kesho utakimbizwa Manispaa ya Shinyanga.

Kauli Mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu (2022) inasema "Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo, Shiriki kuhesabiwa kwa Maendeleo ya Taifa.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Nyanzabara Geraruma, akipiga picha pamoja na Mkurugenzi wa Kituo cha Mafuta Bundala Kishushu (wa pili kutoka kulia), kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko.

Mwenge wa Uhuru ukiwa umewasili mkoani Shinyanga ukitokea mkoani Geita.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post