EMEDO YATAMBULISHA MRADI KUZUIA VIFO VYA WAVUVI... WADAU WAUPOKEA KWA FURAHA

 

Wadau,Wamiliki wa Mitumbwi na Wavuvi wa Kijiji cha Busekera wilayani Bunda Mkoani Mara wameahidi kuchukua tahadhari za kiusalama wanapokuwa katika shughuli zao za uvuvi ili kupunguza ajali za majini na vifo vinavyoweza kuzuilika.


Wametoa kauli hiyo wakati wa utambulisho wa Mradi wa Kupunguza vifo vya Wavuvi vinavyotokana na kuzama maji katika Ziwa Victoria unaofadhiriwa na shirika la Royal National Lifeboat instution kutoka Wingereza na kutekelezwa  na Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO) ulifanyika tarehe 20/06/2022 katika mwalo wa Busekera.


Akizungumza wakati wa  utambulisho wa Mradi huo Diwani wa kata ya Bakumi,Munubi Mussa alipongeza shirika la EMEDO kwa kuwapelekea mradi huo ambao utawasaidia Wavuvi wawezekufanya shughuli zao katika hali ya usalama.


Zawadi Song'ola ambaye ni mmiliki wa Mitumbwi amesema wamekuwa wakichukua tahadhari kabla ya kuingia majini lakini kupitia Mradi huo wa kuzuia ajali za majini kuna haja ya kuongeza vifaa vya uokozi katika Mitumbwi.


Kwa upande wake Meneja mradi kutoka EMEDO Arthur Mugema amesema mradi huo utashirikiana na makundi mbalimbali yanayohusiana na Uvuvi wakiwemo viongozi wa BMU kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiuongozi na kifedha Ili waweze kutatua kero mbalimbali za wavuvi

Naye mkurugenzi wa shirika la EMEDO Editrudith Lukanga amesema hatua ambazo wameanza kuzichukua wadau Wa Uvuvi katika Kijiji Cha Busekera zitapewa nguvu na mradi huo ambao lengo lake ni Kupunguza vifo vya Wavuvi vinavyotokana na kuzama maji.

Amesema pamoja na mambo mengine lakini elimu itatolewa juu ya namna ya kujikinga na ajali za majini ambapo wataalamu watatoa mafunzo ya  kuogelea ,namna ya kujiokoa na kuokoa wengine ajali inapotokea pamoja na kuitumia vifaa vya kujikinga kuzama.

Shirika la EMEDO hadi sasa limeutambulisha mradi huo katika ngazi ya wilaya na sasa mradi umeanza kutambulishwa katika ngazi ya jamii ambako ndiko utekelezaji wake utafanyika.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post