DC NGUVILA ATEMBELEA NA KUKAGUA UTEKELEZAJI WA USAMBAZAJI WA UMEME WA REA MULEBA Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mh. Toba Nguvila (kushoto)

Na Mbuke Shilagi -  Kagera

Katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na idara/taasisi mbalimbali za Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila na wajumbe wa Kamati ya Usalama wa Wilaya wametembelea na kukagua utekelezaji wa usambazaji wa umeme wa REA awamu ya tatu katika vijiji vya Bweyenza, Kangoma na Nyakashenye vilivyopo kata ya Mubunda, wilaya ya Muleba.


Akizungumza wakati wa ziara hiyo, amemtaka Mkandarasi kumaliza kazi kwa uharaka ili wananchi waweze kupata umeme. Pia amemueleza kuwa kiu ya wananchi ni kupata umeme hivyo anatakiwa kuhakikisha anakamilisha mradi mzima kwenye vijiji vyote 30 ndani ya muda aliopewa katika mkataba pasipo kuvuka miezi sita waliyobakiza.


"Ndani  ya siku  14 kwa wale wote ambao watakuwa karibu na nguzo wawashiwe umeme ili waanze kunufaika na umeme kwa sababu  mmenieleza kuwa vifaa vipo, nguzo nimeziona na nyaya zipo hivyo wananchi kazi yenu ni kuunga nyaya majumbani ili wanapofika hapa wanakuwekea mita ili uendelee kuishi kwenye mwanga", amesema Mhe. Nguvila.


Aidha, amemsihi Mkandarasi kutoa taarifa kwa wananchi  endapo kuna ukataji wa miti, migomba, mibuni na mazao mengine kwenye maeneo ambayo wanapitisha nguzo/kwenye njia za kupitisha nguzo ili kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi.


Sambamba na hayo amemtaka Mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anawalipa vibarua stahiki zao kwa wakati huku akiwataka vibarua nao kufanya kazi kwa bidii na uaminifu ili kazi iishe kwa wakati na malengo yaliyokusudiwa yakamilike.


Kwa upande wake mwakilishi wa Mkandarasi wa mradi huo Mhandisi Padon Emmanuel amesema kuwa ndani ya siku 14 vijiji vya Bweyenza, Kangoma na Nyakashenye watawashiwa umeme huku akiahidi kumaliza mradi kwa vijiji vyote 30 ndani ya miezi sita kama alivyosaini katika mkataba.

Paschal Maxmilian mkazi wa kijiji cha Kangoma ameeleza kuwa kwa Serikali kuwapelekea umeme wataondokana na changamoto ya kutumia umeme wa nishati ya jua unaotegemea jua ambapo kipindi cha mvua wanapata changamoto hivyo umeme utakapowashwa wataweza kuchaji simu, kufanya shughuli za uchomeleaji na kuwa na nishati ya mwanga majumbani.


Naye  Jackson Thadeo mkazi wa kijiji cha Kangoma amesema kuwa baada ya kupata umeme itawasaidia kunufaika na umeme huo kwa kueleza kuwa watafungua vibanda vya kunyolea nywele na kazi mbalimbali za kuwaingizia kipato.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments