HATIMAYE KABURI KATIKATI YA BARABARA BARIADI LAONDOLEWA.. FAMILIA YAKUBALI YAISHE


Zoezi la kuhamisha kaburi likiendelea

Na COSTANTINE MATHIAS, Malunde 1 blog Bariadi.

WIKI Moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila kuagiza kuondolowa kwa Kaburi lililokuwa katikati ya Barabara ya Nkindwabiye-Halawa, Familia ya Saguda Madako imetekeleza agizo la kuondoa kaburi hilo huku wakikubali kulipwa fidia ya shilingi laki tano na serikali.


Ikumbukwe kuwa familia hiyo iligoma kuondoa kaburi la Habi Lupigila, kwa madai kuwa hadi walipwe kiasi cha shilingi milioni 30 na kwamba kaburi hilo lilikuwepo eneo hilo tangu mwaka 1975.


Wakizungumza na malunde 1 blog jana mara baada ya kuondoa kaburi hilo baadhi ya ndugu wa marehemu (wana Ukoo) wamesema kaburi hili lilikuwa limejengwa eneo hilo ambalo hapakuwepo na barabara bali ilikuwa sehemu ya barabara.


‘’Tulikuwa tumejenga hapa, tukahama kwenda Matongo, wakati tunajenga hapakuwa na barabara bali lilikuwepo zizi…baadae lilipita barabara, changamoto ni hii ya kuhamisha kwenda kuanza mazishi upya’’’ anasema Susan Mayenga na kuongeza.


‘’Serikali tunaomba ibadilishe sheria kwa ajili ya kulipa fidia, hili tatizo siyo kwetu tu linaweza kutokea kwa wengine, serikali ibadilishe utaratibu wa fidia….kuna gharama za mazishi, usafiri kwa sababu ni msiba mwingine’’ anasema.


Saguda Madako Mayenga anasema mama yake mzazi alifariki tangu mwaka 1975 na kuzikwa katika kijiji cha Nkindwabiye, ambapo kwa sasa limepita barabara linalotoka Byuna-Nkindwabiye hadi Halawa.


Anasema fidia ya shilingi laki tano ambayo wamepatiwa na serikali haitoshi kwa sababu wanahamisha kaburi na kwenda kufanya mazishi upya huku akiiomba kurekebisha sheria ya fidia ili iweze kukidhi mahitaji.

Anaeleza kuwa familia hiyo ilikuwa haijagoma kuhamisha kaburi hilo, bali barabara ilikuwa imelifuata kaburi kwa sababu miaka ya nyuma hapakuwepo na barabara katika eneo hilo.


‘’Tuliiomba serikali ituwezeshe kutoa kaburi, lakini hatukuweza kuelewana, sasa tumekubali tuhamishe, japokuwa laki tano haitoshi kwa sababu tutanunua jeneza, usafiri pamoja na chakula’’ anasema Madako akiongea na malunde 1 blog.

Ng’wamba Susani, mtoto wa Marehemu (Habi Lupigila) anasema serikali imemkumbushia kifo cha mama yake mzazi wakati huo fedha waliyolipwa kwa ajili ya fidia haitoshelezi.

Naye John Ndulu Lupigila ambaye ni msimamizi wa wana Ukoo anasema tukio hilo ni sehemu ya maumivu kwa wana ukoo sababu marehemu alifariki tangu mwaka 1975.

Anasema wana ukoo wamechangishana fedha ili kuweza kufidia gharama za kuhamisha kaburi kutokana na fedha walizolipwa na serikali kutokidhi mahitaji ya zoezi hilo.

Goromondo Isamula mkazi wa Nkindwabiye anasema marehemu alikuwa ameolewa na Madako Amva, alifariki muda mrefu na kaburi hilo lilikuwa kwenye zizi ambapo familia ilijengelea baada ya barabara kupita.


Anaongeza kuwa kaburi hilo lilikuwa njiani, lilikuwa hatari kwa sababu magari yangeweza kugongana na wao kama wananchi wamefurahi kaburi hilo kuondolewa njia sababu barabara imeonekana. 

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nkindwabiye Safari Ng’habi Himbo akizungumza na malunde 1 blog ameishukuru serikali pamoja na wananchi kwa mwitiko wa kushiriki zoezi la kuhamisha kaburi lililokuwa kikwazo katikati ya barabara hiyo.


‘’Niwashukuru ndugu kwa kukubwali wito wa serikali kwa kuondoa kaburi hili lililokuwa adha kwa wakazi wa eneo hilo pamoja na magari, ilikuwa ni shida magari yalikuwa yanasababisha ajali katika eneo hili’’ anasema Safari.


Anaeleza kuwa aliishawishi serikali pamoja na ndugu ili waweze kukubaliana na hatimaye kulitoa kaburi, ‘’nashukuru Serikali upande wa TARURA, wananchi sambamba na ndugu tumekubaliana kutoa mwili kuoka hapa Nkindwabiye kwenda kata ya Matongo’’. anasema.
Jeneza lililobeba mwili wa marehemu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments