MAHAFALI YA KIDATO CHA SITA YA SHULE YA SEKONDARI KAIZELEGE...DC MACHALI ASEMA WATOTO WAPEWE ADHABUMkuu wa Wilaya ya Bukoba Mh. Moses Machali


Na Mbuke Shilagi Kagera.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Moses Machali amewataka wazazi na walezi kuwaadhibu watoto pindi wanapokosea, ili kuwafanya kutambua makosa yao na kujirekebisha.


Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo wakati wa mahafali ya sita ya kidato cha sita ya shule za sekondari Kaizirege na Kemebos zilizoko kata ya Ijuganyondo katika manispaa ya Bukoba.


Amesema kuwa watoto wanapokosea wanapaswa kuadhibiwa kwa viboko au kwa kutumia adhabu nyingine mbadala ili kumkanya asirudie kosa.


"Wazazi wanapaswa kuruhusu hata shuleni watoto waadhibiwe, maana wengine mtoto akiadhibiwa shuleni wanalalamikia walimu bila kujiuliza athari zake, lakini hizo adhabu zisiende kinyume na mwongozo na sheria zilizopo" amesema.


Machali ameongeza kuwa amefanya utafiti na kujua kwamba shule za Kaizirege na Kemebos zinatoa adhabu ya viboko kwa watoto ili kuwafundisha kuwa wakifanya vibaya watapokea tuzo hasi na wakifanya vizuri watapokea tuzo chanya.


"Acheni kuwalea watoto kama kuku wa kisasa, wazazi wenzangu naomba mnielewe, tukifanya hivyo tunawapumbaza watoto wetu, tunawafanya wa kudekadeka na kulialia, matokeo yake tutashindwa kupata Watanzania Wazalendo wenye uwezo wa kulinda na kulitumikia taifa lao", amesema.


Pamoja na hayo ameupongeza uongozi wa Kaizirege na Kemebos kwa kuweka mazingira bora ya wanafunzi kujifunzia, ambayo huwafanya watoto kusoma kwa raha na kwa kujiamini.


Kwa upande wake Meneja wa shule za Kemebos na Kaizirege Eurogius Katiti amewataka wahitimu wa kidato cha sita kuzingatia masomo watakapokwenda vyuoni, badala ya kujiingiza katika starehe.


Aidha Bw. Katiti amesema kuwa shule hizo zimekuwa zikifanya vizuri kitaaluma na kwamba katika matokeo ya mwaka 2021 kwa kidato cha nne wamekuwa wa kwanza kitaifa na kidato cha sita wamekuwa wa pili kitaifa.
Tuzo mbalimbali walizopata uongozi wa Shule za Kemebos na Kaizelege
Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mh. Moses Machali katikati ni Mkurugenzi wa Shule za Kemebos na Kaizelege Yusto Kaizilege na mke wake Elizabeth Kaizelege
Wazazi wakiwa kwenye mahafali
Wahitimu wa kidato cha sita wa shule ya sekondari kaizelege
Meneja wa shule za Kemebos na Kaizelege Eurogius Katiti

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

Post a Comment

Previous Post Next Post