WATATU WAKAMATWA KWA UTOROSHAJI MADINI


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) namna walivyojipanga kudhibiti utoroshaji wa madini mkoani humo.
Meneja Madini Mkoa wa Simiyu Mhandisi Amini Msuya akitoa taarifa kuhusu udhibiti na utoroshaji wa madini mbele ya mkuu wa mkoa wa Simiyu David Kafulila (hayupo pichani).

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila akizungumza na waandishi wa Habari namna walivyojipanga kudhibiti utoroshaji wa madini mkoani humo.

*****

Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.

WATU watatu wamekamatwa kwa tuhuma za utoroshaji wa madini ya dhahabu katika wilaya ya Bariadi mkoa wa Simiyu yenye uzito wa gramu 10, huku Mkuu wa mkoa huo David Kafulila akivitaka vyombo vya Ulinzi na Usalama kuimarisha ulinzi maeneo ya migodi.

Kafulila amewataka Idara ya Madini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi na kufanya ukaguzi maalumu kwenye migodi yote mkoani humo kwa kuwakamata wote wanaojihusisha na utoroshaji wa madini.

Mkuu huyo wa mkoa ameyasema hayo jana (aprili 19, 2022) wakati akiongea Jeshi la Polisi pamoja na Waandishi wa habari, katika kituo cha polisi Bariadi mara baada ya kuwahoji watuhumiwa waliotorosha madini katika mgodi wa Dutwa uliopo Bariadi.

‘’Najua nyie mmetangulizwa, nawatafuta walioko nyuma yenu, mkiwataja mtapata nafuu na msipowataja mtakuwa kafara…watajeni watu wanaowatuma katika mambo hayo, RPC hakikisheni mnafanya ukaguzi maalumu na naamini vyombo mnajua jinsi ya kufanya’’ alisema Kafulila na kuongeza.

"Hawa ambao wamekamatwa tunataka waione rangi ya Rais Samia, kamateni wote kwa sababu hatuwezi kuruhusu hiyo mianya iweze kuwepo, vikosi kazi vilivyoundwa na watu wa usalama hakikisheni mnazibadilisha’’ alisema.

Kwa upande wake Ofisa Madini Mkoa wa Simiyu Mhandisi Amini Msuya alisema walikamata gramu 10.4 mbichi, baada ya kuchomwa zilibaki gramu 7 ambazo zilikuwa hazieleweki zinakoelekea na kwamba watu hao walikamatwa kwa taarifa za kusafirisha dhahabu hizo kwenda nchini Kenya.

Alisema wanashirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha wanafanya uchunguzi kwa watu hao ili kupata mtandao wa utoroshaji wa dhahabu kwa lengo la kuuvunja mtandao huo na pia wanatoa elimu kwa wafanya biashara waweze kufuata taratibu za biashara ya madini.

"Tunafanya uchunguzi kwa watu hawa ili waweze kutupa taarifa, kwa sasa bado ni washukiwa na lengo kubwa ni kuuvunja mtandao katika mkoa wa Simiyu….tunatoa elimu na vikao mbalimbali na wafanyabiashara dhahabu, wafanye biashara katika masoko ya dhahabu ili tuone mwenendo wa soko la dhahabu’’ alisema Mhandisi Msuya.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa polisi Shadrack Majisa alisema jeshi la polisi liko tayari kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kudhibiti utoroshaji wa madini na kwamba wataendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo ya migodi.

Awali Yunis Masuke (ambaye ni mtuhumiwa wa utoroshaji wa dhahabu) alisema yeye ni msimamizi wa mwalo na kwamba alikamatwa kwa tuhuma za kuuza dhahabu grami 10.4 kwa Prisca Seni ambaye naye pia ameshakamatwa.

Naye Gamaya Makoye mlinzi wa mgodi wa EMJ alisema alikamatwa baada ya Yunisi Masuke na Prisca Seni kuuziana dhahabu huku yeye akiwa ni mlinzi wa eneo hilo.

Ofisi ya Madini kwa kushirikina na vyombo vya Ulinzi na Usalama, vinawashikilia Yunis Makoye, Prisca Seni pamoja na Gamaya Makoye wakishukiwa kutorosha au kuuziana dhahabu yenye uzito wa gramu 10 kinyume cha sheria ya madini.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post