ASKOFU BAGONZA : NIMEMFAHAMU BABA WA TAIFA MWL. JULIUS K. NYERERE TOKA NIKIWA MDOGO

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutherani Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe Dkt. Bensoni Bagonza akizungumza kwenye kongamano la maadhimisho ya Miaka 100 ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere


Na Mbuke Shilagi Kagera.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutherani Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe Dkt. Bensoni Bagonza amesema kuwa Mwalimu Julius K. Nyerere, enzi za uhai wake alidumisha Amani, Uhuru, Upendo na Mshikamano, na kuwataka viongozi kumuenzi kwa kuyaishi matendo yake.


Dkt. Bagonza ameyasema hayo akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 100 ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwl. Nyerere, katika kongamano lililofanyika katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.


Amesema kuwa amemfahamu Baba wa Taifa toka akiwa shule ya msingi, na kwamba sio kwa kumsoma bali kwa kufanya naye kazi akiwa kama kiongozi wa jumuiya ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wakati huo, na kuendelea kuwa karibu kwa namna nyingi.


Askofu huyo ameendelea kusema kuwa Baba wa Taifa ameanza uongozi mwaka 1954 mpaka mwaka 1999 akiwa kiongozi mwadilifu, na mtenda kazi, mwenye kupenda wanyonge na kuwatetea.


Amewataka viongozi kuwa wa kwanza kufuata na kuenzi yale yote aliyoyafanya Baba wa Taifa enzi za uhai wake, kuliko kuwaachia wananchi na raia wa kawaida ambaye hajui chochote. 

"Kuweni mfano bora kwa kuyaishi na kuwaelimisha wananchi hasa vijana, ili wayafahamu kwa kina yale yote aliyoyafanya kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla", amesema.


Dkt. Bagonza amesema kuwa Mwl. Nyerere hakwenda shule yoyote kupata elimu ya uongozi, bali alijifunza kupitia Dini, Ukoloni, Vita baridi na Umasikini, ambavyo vilimfanya kuendelea kujifunza na kuwa kiongozi bora.

"Viongozi yaishini yale aliyoyatenda Baba wa Taifa ili kuendelea kumuenzi, hii itasaidia hata vizazi vinavyokuja kuendelea kujifunza zaidi na kujua historia yake na taifa kwa ujumla", amesema.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutherani Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe Dkt. Bensoni Bagonza akizungumza kwenye kongamano hilo.
Mdau wa usafi wa mazingira akitoa mada ya mazingira

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post