WAZIRI DKT MABULA AONYA WANAOTEGESHA KUPATA FIDIA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioongozwa na Mkuu wa wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza Bi. Senye Ngaga alipowasili kwa ajili ya kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza tarehe 21 Machi 2022. Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na uongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi wilayani ya Sengerema mkoani Mwanza kabla ya kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya tarehe 21 Machi 2022.Mkuu wa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza Senye Ngaga akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza tarehe 21 Machi 2022. Kushoto ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Sengerema Yanga Mayanga na wa pili kushoto ni Msajili wa Mabaraza nchini Stella Tullo.

*************************

Na Munir Shemweta, WANMM SENGEREMA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewaonya wananchi wanaojenga au kupanda mazao kwenye maeneo yanayopangwa kutwaliwa na Serikali kwa shughuli mbalimbali zikiwezo za uwekezaji maarufu kama ‘’Tegesha’ mara baada ya kutangazwa tarehe ya ukomo ya kufanya maendelezo.

Dkt Mabula alitoa onyo hilo leo tarehe 21 Machi 2022 wilayani Sengerema mkoani Mwanza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Sengerma.

Alisema, kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wananchi kununua maeneo yaliyopangwa kutwaliwa na serikali kwa ajili ya shughuli mbalimbali na kuanza kufanya maendelezo ya kujenga ama kupanda mazao ili kupata fidia wakati wa zoezi la uthamini huku maeneo hayo yakiwa yametangazwa tarehe ya ukomo ya kufanya maendelezo.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Serikali ya Awamu ya Sita haitavumulia tabia hiyo kwa kuwa jambo hilo linaiingizia hasara serikali na kusisitiza kuwa, wananchi watakaobainika kufanya vitendo vya Tegesha basi watachukuliwa hatua kali ikiwemo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria

‘’Mtu anapanda Mualovela mlimani na inaonekana mualovela wenyewe umechomekwa, nisisitize kuwa, kama kuna kitu kilichoongezeka baada ya kuchukuliwa picha ya anga na kutangazwa kwa tarehe ya ukomo ya maendelezo basi hakitalipwa na serikali italipa kile kinachoonekana kwenye picha ya anga’’ alisema Dkt Mabula

Dkt Mabula alitolea mfano wa eneo la Mlima Nyanzaga uliopo wilayani Sengerema mkoani Mwanza kuwa, kuna baadhi ya wananchi wamenunua eneo la mlima na kuanza kusafirisha migomba nyakati za usiku ili kutegesha kwa lengo la kupata fidia mara tu baada ya kusikia serikali inataka kulitwaa eneo hilo.

Alisema, hali hiyo haiwezi kuvumiliwa hata kidogo na serikali italipa fedha kwa yale maeneo yaliyoonekana katika picha za anga ambazo Wizara ya Ardhi ilizichukua mapema kwa lengo la kuondoa mgongano wakati wa kulipa fidia

Akigeukia uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Sengerema, Dkt Mabula amesema uzinduzi wa baraza hilo umelenga kusogeza huduma kwa wananchi wa wilaya hiyo ya Sengerema ambao awali walikuwa wakiifuata wialayni Geita.

Aliwataka Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi kwenye wilaya ambazo Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya hayajaanza kutoa huduma, kutoa kipaumbele kwa shughuli za mabaraza kwa kutenga maeneo ya ofisi kuwezesha mabaraza kuanza kutoa huduma ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa kwenda kupata huduma katika wilaya nyingine.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments