WAZIRI GWAJIMA AWAONYA WANAOKWAMISHA MIKOPO YA HALMASHAURI, KIVULINI YAMPONGEZA RAIS SAMIA


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amezionya baadhi ya Halmashauri nchini ambazo hazitekelezi kwa haki zoezi la utoaji mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.


Ameyasema hayo Machi 05, 2022 wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza lililofanyika katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Waziri Gwajima amesema zipo Halmashauri nchini zimegubikwa na manung’uniko kwenye utoaji wa mikopo hiyo na hivyo kukwamisha jitihada za Serikali kuwakwamua kiuchumi wananchi.

“Tumesikia manung’uniko kwamba utoaji wa hizo fedha kwenye baadhi ya Halmashauri ni changamoto, watu wanazungushwa, wanapewa kwa kujuana, taarifa hazieleweki na takwimu hazijulikani”, amesema Waziri Gwajima.

“Mhe. Samia Suluhu Hassan atengeneze Sera, wananchi wakatwe kodi, Halmashauri ikusanye, akae mtu mmoja atengeneze utaratibu wa kupindua mambo zisifike kwa walengwa, tusianze kuonana wabaya maana Wizara imeundwa na ufuatiliaji wa Sera utaimarika”, ameonya Waziri Gwajima.

Katika hatua nyingine ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kutoa mikopo ya shilingi bilioni 3.2 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kwa vikundi 1068 vya wanawake vyenye wanufaika 6408 wakiwemo wanawake na kuwasaidia kuboresha shughuli zao na kujitegemea kiuchumi.

Aidha amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakikisha walengwa wa mikopo inayotolewa na Halmashauri wanajengewa uwezo ili mikopo wanayopokea ilete tija badala ya kuitumia katika shughuli zisizokusudiwa ikiwemo wanawake kununua mavazi/madera.

Naye Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amewataka wanawake kujitambua, kujiamini na kunogesha mahusiano katika ndoa zao hatua itakayosaidia kuondokana na migogoro ya kifamilia ambayo huchocheo manyanyaso na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Wasichana KIVULINI, Yassin Ally amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Wizara ya Maendeleo Jamii ambayo itashughulikia changamoto za kijinsia pamoja na kupunguza mzigo mkubwa na kuongeza ufanisi hususani katika kusimamia Mipango, Sera na Mipango yote ya Wizara.

Ally ametumia fursa hiyo kuomba mkakati madhubuti kuwekwa ili kuwanusuru na ukatili watoto wadogo wanaobebwa kwenye mabasi ya shule kwani baadhi ya wasaidizi kwenye magari hayo wamekuwa wakituhumiwa kuwafanyia ukatili wa kingono.

Kilele cha Siku ya Wanawake Duniani hufanyika kila kwaka Machi 08 ambapo mwaka huu kauli mbiu ni “Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu, Tujigokeze Kuhesabiwa”.

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Mkoa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel akizungumza kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akitoa salamu kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza
Mchungaji Theresia Mkami akisoma Risala ya wanawake Mkoa Mwanza ambapo ametoa rai kwa wanaume kuwaamini na kuwawezesha wanawake katika shughuli za kiuchumi ili kuongeza pato la kaya huku akisema mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri imeleta tija kubwa katika jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Wasichana KIVULINI, Yassin Ally (kushoto) akiwa kwenye maandamano wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza
Mabango yenye ujumbe mbalimbali 
 Waendesha bodaboda wakiwa kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Wasichana KIVULINI, Yassin Ally (kulia) akiwa kwenye maandamano wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima (katikati) akipokea maandamano wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima (katikati) akicheza wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima (katikati) akicheza ngoma za asili wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza
Watoto wakitoa ujumbe wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya Mkoa Mwanza

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post