KATAMBI ASHIRIKI IBADA MAALUMU KUOMBEA WANAWAKE KANISA LA ANGLIKANA SHINYANGA


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na Viongozi wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT) pamoja na Waumini aliposhiriki katika ibada maalum ya maombi ya kuombea Wanawake katika Kanisa la Anglikana, Lubaga Mkoani Shinyanga kuelekea siku ya Wanawake Duniani Machi 8.
Washiriki wakisikiliza kwa makini hotuba ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini.
Washiriki wakisikiliza kwa makini hotuba ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini .

**
Na Mwandishi wetu - SHINYANGA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi ameshiriki katika ibada maalum ya maombi ya kuombea Wanawake katika Kanisa la Anglikana, Lubaga Mkoani Shinyanga kuelekea siku ya Wanawake Duniani Machi 8.

Naibu Waziri Katambi akiwa katika ibada hiyo ameipongeza Jumuiya ya Kikristo ya Tanzania “Christian Council of Tanzania” (CCT) kwa namna imekuwa jukwaa muhimu la kuunganisha Wanawake kiroho, kiakili na kimwili ambapo imekuwa ni nyenzo muhimu sana katika ujenzi wa misingi ya maadili, familia, jumuiya na Taifa lenye watu wenye hofu ya Mungu, utu, uzalendo na uwajibikaji.

“Jumuiya hii imekuwa na mchango mkubwa katika kujenga umoja na mshikamano kwa jamii ili iwe na ustawi imara kuanzia ngazi ya familia hali itakayosaidia kuondoa changamoto zinazotokana na matukio mbalimbali ya ukatili wa kijinsia kwa kuwa na Taifa lenye watu wenye hofu ya Mungu,” alieleza.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwa na mikakati Madhubuti ya kutokomeza changamoto zinazotokana na matukio ya ukatili wa kijinsia, mauaji holela ya wanawake, mimba na ndoa za utotoni.

Sambamba na hayo, amewaomba Viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa kuendelea kudumisha amani na umoja.

Kwa Upande wake Askofu wa Kanisa hilo la Dayosisi ya Shinyanga, Jonhson Chinyongole alisema kuwa lengo la Jumuiya hiyo ya Kikristo nchini ilianzishwa kwa lengo la kujenga umoja kati ya makanisa wanachama katika mambo mbalimbali ikiwemo elimu, afya, mazingira, uchechemuzi na sera, mahusiano kiamani, maendeleo ya wanawake, amani na haki.

Awali akisoma risala, Bi. Terra Mongela alisema kuwa umoja huo umewasaidia kuwa sehemu ya kutekeleza maono ya Serikali kupitia mikakati yake mbalimbali hasa Mkakati wa kuzuia Ukatili dhidi ya Wanawake na Wazee (MTAKUWWA) na Mkakati wa Kitaifa wa kutokomeza Mauaji ya Wazee pamoja na Mkakati wa Mkoa wa Kuzuia ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments