MAHAFALI YA 32 KIDATO CHA 6 SHULE YA WASICHANA BWIRU YAFANYIKA....WALIA UKOSEFU WA UZIO


Mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI Yassin Ally (kulia) akikabidhi vyeti kwa wahitimu.
Uongozi wa Shule ya Sekondari ya Bwiru Wasichana iliyopo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza umeeleza kuwa ukosefu wa uzio katika mabweni unahatarisha usalama wa wanafunzi wa Shule hiyo na hivyo kuomba Serikali na wadau mbalimbali kusaidia kutatua changamoto hiyo.


Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Mecktrida Shija ameyasema hayo Machi 31, 2022 wakati akizungumza kwenye mahafali ya 32 ya wanafunzi wa kidato cha sita ambapo wanafunzi 411 wanatarajia kuhitimu mwaka huu.


Mwl. Shija amesema kupitia mapato ya ndani, uongozi wa shule hiyo umeanza kujenga uzio wa tofali kuzungunga mabweni hatua itakayosaidia kuimarisha usalama wa wanafunzi kutokana na kuwa jirani na Ziwa Victoria hali inayochochea mwingiliano wanafunzi na wananchi hususani wavuvi.


Pia Mwl. Shija ameeleza kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vitano vya madarasa, nyumba za waalimu unaoambatana pia na uchakavu wa nyumba zilizopo pamoja na uhaba wa waalimu wa masomo ya Sayansi ikiwemo Fizikia na Kemia.


Katika hatua nyingine Mwl. Shija ametoa shukurani kwa shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI kwa kuchangia maendeleo shuleni hapo ambapo mwaka 2017 shirika hilo lilitoa vyerehani 15 na vifaa vilivyoanzisha mradi wa kiwanda cha kushona sare za wanafunzi hatua iliyosaidia Shule kupata faida takribani shilingi milioni 20 na kuanzisha ujenzi wa uzio.


Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, Carolin Saro aliomba changamoto ya ukosefu wa uzio kutafutiwa ufumbuzi kwani inawatatiza kimasomo hususani nyakati za usiku wanapotakiwa kwenda kwenye kujisomea.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo ameendesha harambee ya papo kwa hapo na kusaidia upatikanaji wa tofali 1,560 kati ya hizo yeye akitoa tofali 1,000, fedha taslimu shilingi 182,500, ahadi shilingi 2,0050,000 pamoja na mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi wa uzio shuleni hapo.


Aidha Yassin ametoa rai kwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Wizara ya OR-TAMISEMI kuandaa mkakati wa kuaandaa wahitimu wa kidato cha nne na kidato cha sita ili kipindi cha likizo wajitolee kufundisha katika Shule za Msingi na Sekondari hatua itakayosaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa waalimu lakini pia ukosefu wa uzoefu kazini wanapohitimu vyuoni na kuingia kwenye soko la ajira.


Pia ametoa rai kwa wazazi na walezi kuwapa stadi za maisha watoto wao katika kipindi cha likizo kwa kuwafundisha shughuli mbalimbali za nyumbani ikiwemo ujasiriamali, kilimo ama kujihudumia wakiwa nyumbani hatua itakayowasaidia kujitambua na kujilinda katika kipindo cha kusubiri matokeo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bwiru Wasichana, Mwl. Mecktrida Shija akizungumza kwenye mahafali hayo.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally akizungumza kwenye mahafali hayo ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Mwanafunzi Carolin Saro (katikati) akisoma risala ya wahitimu wa kidato cha sita Shule ya Sekondari Bwiru Wasichana.
Wahitimu wakitoa burudani kwenye mahafali hayo.
Mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI Yassin Ally (kulia) akikabidhi vyeti kwa wahitimu.
Wanafunzi na wageni wakifurahia burudani ya ngoma za asili kwenye mahafali hayo.
Wanafunzi wakitoa burudani yenye mahadhi ya kidigitali kwenye mahafali hayo.
Wahitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Wasichana Bwiru.
Wahitimu wakitoa burudani.
Mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI Yassin Ally (kushoto) akitoa nasaha kwa wahitimu ili kujilinda wakati wakisubiri matokeo ya mtihani.
Mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI Yassin Ally (kulia) akimkabidhi zawadi Mkuu wa Shule ya Sekondari Bwiru Wasichana Mwl. Mecktrida Shija kwa ufanisi mzuri kazini.
Watumishi wa Shule ya Sekondari Bwiru Wasichana.
Shule ya Sekondari Bwiru Wasichana ilianzishwa 1957 na mwaka 1990 ikaanza kuchua wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na sita kwa masomo mbalimbali ikiwemo PCB, PCM, HGE, HGK, EGM, HKL na CBG. Katika mtihani wa kidato cha sita mwaka 2021 kulikuwa na wahitimu 449 ambapo waliopata daraja la kwanza ni 93, daraja la pili 225, daraja la tatu 129 na daraja la nne wawili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post