MAADHIMISHO YA MIAKA 100 YA KUMBUKIZI YA KITAIFA KUZALIWA MWALIMU JULIUS NYERERE KUFANYIKA APRILI 2022


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imepitisha mpango wa Chama hicho kuhusu kuadhimisha ya kumbukizi ya Kitaifa ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ,lengo kukumbusha kazi kubwa na nzuri aliyoifanya katika Nchi ya Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka,alisema dhima ya Chama hicho kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 100 ya kuzaliwa Nyerere aliyezaliwa Aprili 13 Mwaka 1922, imetokana na chama hicho kutambua mchango uliofanywa na kiongozi huyo katika ujenzi wa Taifa.

“Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imeridhia na kuekeleza kufanyika kwa mdahalo wa kitaifa ambao utakumbushia mema na mazuri yake kwa kuzingatia tulipotoka, tulipo na tunapoelekea huku tukitafakari kama Taifa namna ambavyo tunaendelea kuishi katika nadharia ya kiongozi wetu huyo mashuhuri,"amesema Shaka.

Amefafanua kwamba mwaka 2022 ,wataadhimisha kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa kiongozi mahiri ,mzalendo na mwanamapinduzi wa kweli Mwalimu Julius Nyerere Baba wa Taifa.Mwenyekiti wa kwanza wa TANU na CCM na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,aliyezaliwa Aprili 13,1922 katika Kijiji cha Mwitongo Wilayani Butiama mkoani Mara.

Alifariki dunia Oktoba 14,1999 ambapo fikra zake,utu ,uongozi na mchango wake usiokifani katika maisha ya Watanzania na nchi nyingi za Bara la Afrika bado matendo yake yanaendelea kuishi akiwa mpigania Uhuru wa Afrika, mwanasiasa mahari,mwanafamilia mpenda maendeleo ya watu,Mchumi,msomi na mwanafalsafa.

"Hadi leo Tanzania na jumla kwa ujumla inamkumbuka Mwalimu Julius Nyerere kabla na baada ya Uhuru wa Tanganyika na hatimaye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26 ,1964 kutokana na utumishi wake iliotukuka .Kamati Kuu ya Halmashauri ya CCM Taifa imeridhia na kuelekeza kufanyika kwa mdahalo wa Kitaifa ambao utakumbushia mema na mazuri yake kwa kuzingatia tulipotoka,tulipo na tunakoelekea huku tukitafakari kama Taifa namna ambavyo tunaendelea kuishi katika nadharia za kiongozi wetu mashuhuri Mwalimu Julius Nyerere.

"Mdahalo utafanyika siku ya Aprili 9 katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Kibaha na utahudhuriwa na wanazuoni wabobezi wa masuala ya siasa, Uchumi, uongozi na utawala,baadhi ya watu mashuhuri waliofanya kazi na Mwalimu ,vijana na makund rika kike na kwa kiume ,viongozi na watendaji wa Serikali, Taasisi za elimu ya juu, taasisi za fedha na mashirika yasiyo ya kiserikali , viongozi wa dini pamoja na Taasisi zinazosimamia maendeleo ya Sayansi na Teknolojia."

Shaka amesema katika kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere kwa kizazi cha sasa na baadae Kamati Kuu imeeleeza mawasilisho yote yatakayotolewa yatakuwa ni mali ya Chama ambayo yatatumika kuandika na kuweka kwenye maktaba ya kudumu itakayokuwa na sehemu muhimu itakayotambulika Kama "Miaka 100 ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Mwalimu J.K.Nyerere."

"Kwa kuzingatia umuhimu wa kutunza na kuenzi kumbukizi muhimu za viongozi wakuu waliotuletea ukombozi Kamati Kuu imeeleeza kuendesha mdahalo wenye maudhui Kama haya kwa Hayati Abeid Aman Karume Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti w Baraza la Mapinduzi,Mwanapinduzi wa kweli aliyeuwawa na wapinga maendeleo Aprili 7,1972 Kisiwandui Mjini Zanzibar ambapo mwaka huu Hayati Abeid Amani Karume anatimiza miaka 50 tokea kuuawa kwake na wapinga maendeleo."

Katika hatua nyingine Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuunda Tume kufuatilia matukio mbalimbali ya uhalifu na kisababisha baadhi ya Watanzania kuuwawa katika Mkoa wa Mtwara na Tanga wilayani Kilindi.

"Kamati Kuu imeelekeza Serikali kuangalia upya mwenendo wa Jeshi la Polisi nchini ambao umekuwa hauridhishi na kulalamikiwa na Wananchi kutokana na matendoe yanayofanywa na baadhi ya maofisa na askari wa Jeshi hilo kinyume na muongozo wa utendaji kazi wa Jeshi la Polisi,"amesema Shaka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments