MIKUTANO YA HADHARA YA VYAMA VYA SIASA YANUKIA...RAIS SAMIA AAGIZA KANUNI ZIANDALIWE


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametoa agizo kwa Waziri wa Katiba na Sheria kuandaa kanuni zitakazoelezeka jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ambayo kwa muda mrefu ilikuwa imezuiwa.

Rais Samia ametoa maelekezo hayo baada ya kupokea maazimio ya awali kutoka kwa kikosi kazi alichokiteua cha kufuatilia hoja zilizojitokeza katika mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa uliofanyika Dodoma, Desemba 15 hadi 17, 2021.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa mawasiliano ya rais ikulu, Zuhura Yunus imeeleza kuwa Rais Samia amemwagiza waziri huyo wa katika na sheria kushikirikiana na Tanganyika Law Society (TLS) na Zanzibar Law Society (ZLS) kutengeneza kanuni hizo.

Kikosi kazi hicho chenye wajumbe 24, na ambacho kinawajibika moja kwa moja kwa Rais, kiliwasilisha maazimio hayo ikulu jijini Dodoma ambayo yamegawanywa katika makundi matatu ya muda wa utekelezaji.

Azimio la muda mfupi ni uandaaji wa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Baadhi ya maazimio ya muda wa kati ni pamoja na rushwa na maadili katika uchaguzi, ruzuku, elimu ya uraia huku masuala yanayohusu uchaguzi na katika mpya vikiwa ni mpango wa muda mrefu.

Rais amekutana na kuzungumza na kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kinachoongozwa na mwenyekiti wake, Profesa Rwakaza Mukandala, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post