MCHUNGAJI WA KANISA ALIYEZUA TAHARUKI 'KUFUFUA WAFU' SHINYANGA AKAMATWA...'MSUKULE MCHONGO' NAYE ADAKWA


Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando
****
JESHI la Polisi Mkoani Shinyanga linamshikilia Mchungaji wa Kanisa CRTC, Yohana Nyasilu (34) akituhumiwa kwa kosa la kudai anafufua watu waliokufa kwa lengo la kuvuta watu katika kanisa lake ili lipate waumini wengi.

Mbali ya mchungaji huyo pia Jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Yohana Komanya (21) ambaye hata hivyo makazi yake hayakufahamika mara moja kwa kujifanya Msukule aliyefufuliwa na Mchungaji huyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP George Kyando Mchungaji huyo amekamatwa kwenye kijiji na kata ya Puni wilayani Shinyanga baada ya taarifa za kuwepo kwa mtu anayefufua watu kufikishwa polisi.

Kamanda Kyando amesema baada ya taarifa za mchungaji huyo kufikishwa Polisi, walikwenda katika kata hiyo ambako umati wa watu walikuwa wamekusanyika kushuhudia miujiza ya kufufua wafu iliyokuwa ikifanywa na mchungaji huyo.

“Ni kweli jamii ya watu wengi wa kijiji cha Puni walitaharuki, walijaa sana kushuhudia kile alichokuwa akikifanya na waliamini ni mtu mwenye uwezo wa kufufua wafu, hata hivyo mtu aliyedaiwa kufufuliwa baadaye alimgeuka mchungaji kwa kudai alimshawishi adai kwamba alikuwa amekufa na kufufuliwa na Mchungaji huyo wa Kanisa",amesema Kamanda Kyando.

“Lengo lake lilikuwa kuvuta watu wengi na kiini cha kupata watu wengi kanisani ni kupata sadaka nyingi, nia ni kipato, hivyo tunamshikilia mchungaji huyu na uchunguzi ukikamilika jalada litapelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali kuona wachungaji wa namna hii wanachukuliwa hatua gani,” ameongeza Kamanda Kyando.

Kamanda Kyando ametoa wito kwa watu wa madhehebu yote ya dini kujihadhari na uongo na udanganyifu unaoweza kuwaletea taharuki kwenye jamii na kwamba tayari jamii ya watu wa Puni ilishataharuki na kuamini kweli mchungaji huyo alikuwa na uwezo wa kufufua wafu.

“Jeshi la Polisi kwa upande wetu hatutaacha kuwashughulikia watu wa dini wa aina hii maana yake kuleta taharuki kwenye jamii yetu ni kitu ambacho hakiruhusiwi kwenye jamii yetu, na kwa taarifa nilizonazo tukio hili si la mara ya kwanza kwa mchungaji huyu,” ameeleza Kamanda Kyando.

Tazama Video hapa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post