CCM WATAKA JESHI LA POLISI LIANGALIWE UPYA...MAKONDA AIBUKA


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka


Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, imeielekeza serikali kuangalia upya mwenendo wa jeshi la polisi nchini ambao umekuwa ukilalamikiwa na wananchi.

Taarifa hiyo imetolewa leo Machi 12, 2022, na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka, jijini Dar es Salaam, ambapo pia kamati hiyo imempongeza Rais Samia kwa hatua alizozichukua kufuatia mauaji yaliyofanyika mkoani Mtwara na Tanga.

"Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, imeielekeza serikali kuangalia upya mwenendo wa jeshi la polisi nchini ambao umekuwa ukilalamikiwa na wananchi kutokana na matendo yanayofanywa na baadhi ya maafisa kinyume na miongozo ya utendaji wa kazi," amesema Shaka.

Baada ya CCM kutaka kuundwa kwa kamati ya kulichunguza Jeshi la Polisi kufuatia malalamiko mengi ya Watanzania, Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda , ameibuka katika ukurasa wake wa Instagram na kusema yupo tayari kutoa ushahidi mbele ya kamati hiyo.

Makonda ambaye kuwa kimya kwa muda mrefu huku akiandamwa na mzimu wa kutaka ashtakiwe leo ameamua kuvunja ukimya Kwa kuandika juu ya uonevu unaofanywa na Jeshi la Polisi.

"Naunga mkono hoja ya kamati kuu, ya kuchunguza mwenendo wa baadhi ya maafisa wa jeshi la polisi, wanaolipaka tope jeshi la polisi kwakuwalinda wafanyabiashara MATAPELI wanaodhulumu mali za watu. Naomba tuanze na Dar es salaam na mimi PAUL MAKONDA niko tayari kutoa ushirikiano" ameandika Makonda .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post