WAZIRI GWAJIMA AZINDUA KITUO CHA WATOTO KATIKA SOKO LA MIRONGO MWANZA


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima (wa tano kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kituo cha Malezi na Makuzi kwa Watoto kilichopo katika soko la wafanyabiashara wadogo Mirongo jijini Mwanza.

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amezindua rasmi Kituo cha Malezi na Makuzi kwa Watoto Mirongo kilichopo katika soko la wajasiriamali Mirongo jijini Mwanza na kutoa rai kwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kukisimamia vyema Kituo hicho.

Uzinduzi huo ulifanyika Februari 09, 2021 ambapo ujenzi wa Kituo hicho ulienda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya Soko la Mirongo ambayo ni pamoja na vyoo, mitaro na mabanda mawili ya kufanyia biashara na ujenzi wa visimba ambao unaendelea hivyo kuondoa adha kwa wajasiriamali katika soko hilo ambalo ni maarufu kwa bidhaa za mbogamboga na matunda.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Gwajima alisema Serikali inaandaa mfumo utakaosaidia malezi na makuzi kwa ajili ya watoto hatua itakayosaidia kuwakinga na vitendo vya ukatili wa kijinsia na hivyo kupingeza hatua ya ujenzi wa kituo hicho katika soko la Mirongo kwani kitasaidia jitihada za malezi bora kwa watoto.

Naye Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi alisema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Kituo hicho, Serikali itasaidia upatikanaji wa waalimu walezi watakaokuwa na jukumu la uangalizi wa watoto watakaokuwa kituoni hapo pindi wazazi wao watakapikuwa kwenye shughuli za biashara.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally alisema utafiti uliofanywa na shirika hilo ulibaini kuwa asilimia zaidi ya 60 ya wafanyabiashara wadogo masokoni ni wanawake na wanakumbana na changamoto za malezi ya watoto wanapokuwa kwenye biashara na hivyo kuja na wazo la ujenzi wa Kituo hicho ili kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo.

Maboresho hayo yaligharimu shilingi milioni 88 ambapo shirika la kutetea haki za wanawake na watoto KIVULINI kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo I4IF, UKAid, IrishAid limetoa shilingi milioni 60 huku Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikitoa shilingi Milioni 20.

Miundombinu bora katika soko la Mirongo itasaidia wajasiriamali kufanya biashara zao katika mazingira salama na kukuza biashara zao huku Kituo cha Malezi na Makuzi kwa Watoto kikisaidia kuimarisha usalama wa watoto pindi wazazi wao wanapokuwa kwenye biashara huku pia akina mama wanaonyonyesha wakiwa na eneo maalum la kunyonyeshea.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Kituo cha Malezi na Makuzi kwa Watoto Mirongo jijini Mwanza.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima (katika) akimpongeza Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally (kulia) kwa kusaidia ujenzi wa Kituo cha Malezi na Makuzi kwa Watoto Mirongo ambapo shirika lake kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo limetoa shilingi milioni 68 na Halmashauri ya Jiji la Mwanza Milioni 20 na kusaidia uboreshaji wa miundombinu katika soko la wajasiriamali Mirongo pamoja na ujenzi wa Kituo hicho.
Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi (katikati) akizungumza kwenye uzinduzi wa Kituo hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel (hayuko pichani).
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto KIVULINI, Yassin Ally akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kituo hicho ambapo alisema kitasaidia pia wanawake wajasiriamali katika soko la Mirongo kupata eneo maalum kwa ajili ya kunyonyeshea.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima (wa kwanza kushoto) pamoja na viongozi mbalimbali jijini Mwanza akizindua rasmi Kituo cha Malezi na Makuzi kwa Watoto Mirongo jijini Mwanza.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima (katikati) akimsaidia kubembea mmoja kati ya watoto walio katika Kituo cha Malezi na Makuzi kwa Watoto Mirongo kilichojengwa katika soko la wajasiriamali Mirongo jijini Mwanza. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya Nyamagana Amina Makilagi na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI Yassin Ally.
Baadhi ya akina mama wajasiriamali katika soko la Mirongo jijini Mwanza wakiwa na watoto wao katika Kituo cha Malezi na Makuzi kwa Watoto Mirongo wakati wa uzinduzi rasmi wa Kituo hicho.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima (katikati) akiwasili katika viunga vya soko la Mirongo kwa ajili ya uzinduzi wa Kituo cha Malezi na Makuzi kwa Watoto. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya Nyamagana Amina Makilagi na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI Yassin Ally.
Wanawake wajasiriamali katika soko la Mirongo wakimkaribisha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima (hayuko pichani).
Wanachi waliojitokeza kwa ajili ya uzinduzi wa Kituo hicho.
Wakazi wa jiji la Mwanza wakishuhudia uzinduzi wa Kituo cha Malezi na Makuzi kwa Watoto Mirongo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima pia alikutana na Kamati za MTAKUWWA ngazi za Mitaa katika jiji la Mwanza na kuwahimiza wajumbe Kamati hizo kuwajibika ipasavyo ili kuzuia vitendo vya Ukatili wa Kijinsia kutokea katika Mitaa yao.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wajumbe wa Kamati za MTAKUWWA ngazi za Mitaa katika jiji la Mwanza.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima (hayuko pichani) pia alikutana na wajumbe wa Kamati ya MTAKUWWA ngazi ya Mkoa Mwanza (pichani) kwa ajili ya kupeana mikakati mbalimbali ya kupambana na Ukatili wa Kijinsia ambapo aliipongeza Kamati hiyo kwa kufanya jitihada kubwa kupamabana na Ukatili wa Kijinsia.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima alikutana pia na viongozi wa Machinga Mkoa Mwanza na kuagiza viongozi wa Serikali mkoani Mwanza kukutana na makundi yote mawili (Shirikisho la Machinga Tanzania na Muungano wa Machinga Mkoa Mwanza) kuja na mikakati ya kupata shirikisho moja la linakalowaunganisha machinga wote.
Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Ngusa Samike akizungumza kwenye kikao baina ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima (hayuko pichani) na wajumbe wa Kati ya MTAKUWWA ngazi ya Mkoa Mwanza.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima pia alitembelea Chuo cha Maendeleo ya Jamii na Ufundi Misungwi (CDTTI) na kuwahimiza wanafunzi wa Chuo hicho kuwa wabunifu na kutumia vyema taaluma wanayoipata kujiajiri na kuajiriwa ili kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika jamii.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na uongozi na wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Misungwi (CDTTI).
Tazama Video hapa chini

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments