JE UNATAKA KUTUMA PESA?? KUWA MAKINI


Kabla kutuma pesa, kujiridhisha muhimu,
Isije ikawa pesa, utumako hufahamu,
Ukatuma kimakosa, na hali ikawa ngumu,
Epuka hiyo hasara, zingatia masharti.

Huduma nyingi za pesa, mifumo yao muhimu,
Wakati watuma pesa, hatua zamu kwa zamu,
Hatua siyo anasa, kuzingatia muhimu,
Epuka hiyo hasara, zingatia masharti.

Watu hupoteza pesa, nakushindwa kujikimu,
Umakini wanakosa, ambao kwetu muhimu,
Kuhakiki wanakosa, kujikuta hali ngumu,
Epuka hiyo hasara, zingatia masharti.

Huduma za tuma pesa, hatua zake muhimu,
Twatoa kwako hamasa, ni vema uzifahamu,
Haraka haraka sasa, utapata hali ngumu,
Epuka hiyo hasara, zingatia masharti.

Wakati watuma pesa, uangalifu muhimu,
Ili uwe wa kisasa, hatua zote muhimu,
Usije kuzua visa, kuibiwa iwe zamu,
Epuka hiyo hasara, zingatia masharti.

Kama unatuma pesa, kwa hatua zote humu,
Huwezi fanya makosa, ukaipoteza hamu,
Usalama zako pesa, unabakia mtamu,
Epuka hiyo hasara, zingatia masharti.

Kwa nani watuma pesa, jina hilo ni muhimu,
Endapo umelikosa, utatambua kwa zamu,
Tarudia tuma pesa, litoke walifahamu,
Epuka hiyo hasara, zingatia masharti.

Ukiyafanya makosa, hatua uzifahamu,
Taarifu M-Pesa, na Tigo-Pesa muhimu,
Hata wale HaloPesa, Airtel Money humu,
Epuka hiyo hasara, zingatia masharti.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments