MAHAKAMA YAAMURU MAKONDA ASAKWE MPAKA KOROMIJE



Mahakama ya hakimu mkazi Wilaya ya Kinondoni imekubali maombi ya upande wa waleta maombi katika kesi namba 1 ya mwaka 2022, iliyofunguliwa dhidi ya aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda kutafutwa kwenye makazi yake ya Dar es salaam na kijijini kwao Koromije Misungwi mkoani Mwanza.

Katika kesi hiyo Wakili wa upande wa Serikali Deis Makakala anawawakilisha DPP na DCI, huku wakili Jarome Kicherere pamoja na Wakili Hekima Mwasipu wakimwakilisha Said Kubenea. Wakili Kicherere ameeleza mbele ya mahakama kwamba wameshindwa kumpata mjibu maombi namba 3 ambayo ni Paul Christian Makonda.

Wakili akaendelea kueleza kuwa alikokuwa anakaa maeneo ya Masaki jijini Dar es salaam amehama, na pia wamepata mawasiliano yake ya simu ambayo ni namba ya simu ya 0683009009, vilevile namba hiyo haipatikani na kutokana na hivyo wameomba mahakama kuwapa hati ya wito ili waweze kumtafuta kwenye maeneo mbalimbali na hiyo ni ( kwa mujibu wa kifungu cha 103 cha sheria ya mwenendo ya makosa ya Jinai CPA).

Aidha Wameomba kupewa hati za wito moja watapeleka alipokuwa akifanya kazi kwa mara ya mwisho, kwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, nyingine ipelekwe kwenye nyumba aliyokuwa anaishi kwa mara ya mwisho na nyingine ipelekwe kwenye maeneo anayotembelea mara kwa mara kwenye duka la Horzonal Pharmacy Morocco.

Aidha, barua nyingine ya wito iwekwe katika uwanja wa ndege wa Mwalim Julius Nyerere, nyingine Ipelekwe bandarini, huku nyingine ipelekwe Kolomije, Misungwi mkoani Mwanza na ya mwisho ipelekwe kwenye gazeti moja la Kiswahili na jingine la Kiingereza.

Wakili akaongeza kuwa lengo lao ni Mjibu maombi Paul Makonda apate taarifa juu ya uwepo wa kesi hiyo Mahakamani. Wakili Deis aliyekuwepo mahakamani ameeleza kuwa yeye anamwakilisha DPP na DCI hivyo hawezi kutoa majibu yoyote kuhusu mjibu maombi namba 3.


Hakimu Aron Ryamuya ameeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu hicho cha 103 alichokisoma na wakili Kicherere, kuwa kwenda kubandika katika viwanja vya ndege na bandarini ni kinyume cha sheria na ni uchafuzi wa mazingira.


Hivyo Hakimu akakubali tangazo hilo lipelekwa nyumbani kwake Masaki na kwenye gazeti pekee, huku maombi ya tangazo hilo kupelekwa kwenye maeneo hayo mengine yaliyosalia yakitupiliwa mbali.


Upande wa waleta maombi Wakaomba pia wakabandike tangazo hilo na kijijini kwao Koromije, akieleza huenda yupo kijijini kwao, ombi ambalo lilikubaliwa na hakimu. Kesi hiyo imeahirishwa hadi jumatatu ya Machi 2, 2022 ambapo siku hiyo ndio kesi hiyo itatajwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments