WAZIRI BASHUNGWA APENDEZWA NA CWT KINAVYOCHOCHEA UBORA WA ELIMU NCHINI, ASIFU MPANGO WA ELIMU BURE

Na Dotto Kwilasa Malunde 1 blog-DODOMA

SERIKALI kupitia Wizara ya Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)imesema imepeleka jumla ya shilingi trilioni 1.43, kwa ajili ya kugharamia Mpango wa elimu msingi bila Malipo ulioanza kutekelezwa 2015 na kuleta fursa ya upatikanaji wa elimu kwa kuongeza uandikishaji wa wanafunzi, kutokana na kuondolewa kwa vikwazo. 

Hayo yameelezwa na Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa Februari 11,2022 jijini hapa katika hafla ya  utoaji tuzo  za ubora wa taaluma kwa walimu,wanafunzi , Shule, Halmashauri na mikoa yote  iliyofanya vizuri kwenye matokeo  ya mitihani ya Mwaka 2021 ya kumaliza elimu ya msingi, kidato cha nne na kidato cha sita.

Amesema katika mwaka 2016, jumla ya wanafunzi 2,670,125 waliandikishwa, kati ya hao wanafunzi 917,137 wa elimu ya awali, 1,386,592 wa darasa la kwanza na wanafunzi 366,396 wa kidato cha kwanza.

Waziri Bashungwa ameeleza mwaka 2022, jumla ya wanafunzi 3,046,919 wameandikishwa, kati ya hao wanafunzi 1,123,800 ni wa Elimu ya Awali sawa na asilimia 82, wakiwemo wenye mahitaji maalum 2,352, wanafunzi 1,454,544 ni wa darasa la kwanza sawa asilimia 91, huku wanafunzi 664,698 wakiwemo wenye mahitaji maalum ni 2,747.

"Wanafunzi 664,698 wa kidato cha kwanza wameripoti shuleni, sawa na asilimia 73.2 ya wanafunzi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza Mwaka 2022, wakiwemo wanafunzi 679 wenye mahitaji maalum,"amesema.

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na walimu nchini katika kuboresha taaluma, hivyo ni dhamira ya Serikali kuendelea na ujenzi wa nyumba za walimu kulingana na bajeti.

"Serikali ya awamu ya Sita imeendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika Shule za Msingi na Sekondari Nchini,kwa Mwaka 2021 ufaulu katika mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi umefikia asilimia 81.97, mtihani wa kumaliza kidato cha nne umefikia asilimia 87.30 na kidato cha sita asilimia 99.62.

“Ninawapongeza walimu kupitia CWT kwa kuongeza na kuimarisha ufaulu,hata hivyo nina wahimiza kuongeza usimamizi wa shughuli za Elimu na kuondoa changamoto zinazosababisha baadhi ya shule kutofanya vizuri”amesisitiza Waziri huyo.

Katika kuimarisha utendaji kazi, Bashungwa ameeleza kuwa mipango madhubuti imewekwa ili kuhakikisha walimu, wakuu wa shule, Maafisa Elimu wa Kata, Wilaya na Mikoa wanaendelea kupata mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo katika ufundishaji na usimamizi wa Sekta ya Elimu.

Amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya walimu 1,817 wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum ya ujifunzaji, wamejengewa uwezo wa kutumia mbinu za kufundishia na kujifunzia. 

Vilevile walimu Wakuu 8,096 walipata mafunzo juu ya matumizi ya Kiunzi cha Uthibiti Ubora wa Shule ili kuhakikisha Uthibiti wa Ubora wa Shule unakuwa na matokeo mazuri, kuanzia katika ngazi ya Shule na kwamba mafunzo kama hayo yataendelea kutolewa kila mwaka ili kutimiza lengo la kumarisha utendaji kazi.

Pamoja na hayo amezielekeza Taasisi za elimu nchini kuhakikisha wanafuata sheria, miongozo na taratibu katika usimamizi wa sekta ya Elimu ili kufikia malengo ya Serikali ikiwa ni pamoja na kusimamia vizuri miradi yote, inayotekelezwa katika maeneo yao, ili kuwa na miradi yenye viwango vinavyoendana  na thamani ya fedha.

Vile vile amesema Serikali itaendelea kutoa Elimumsingi bila malipo, kuboresha miundombinu, na kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa Chama Cha Walimu  Tanzanaia (CWT )Mwalimu  Deus Seif amesema Chama hicho kinatambua  jitihada  kubwa zinazofanywa na walimu nchini katika kuhakikisha wanafunzi wanapata ufaulu mzuri.

Kutokana na hayo Katibu huyo kupitia CWT ameahidi kushirikiana na Serikali kuendelea kutatua kero zinazowakabili walimu ili kuwapa ari ya kufanya kazi katika mazingira mazuri.

“Tunatambua Serikali inaendelea kutujali kupitia upandishwaji wa madaraja na  urekebishwaji wa mishahara kwa walimu, pamoja na malimbikizo ya madeni  yasiyo ya mishahara,hivyo na sisi Kwa nafasi yetu tutaendelea kushirikiana Katika kutatua kero nyingine ”amesema Mwl Seif.

Amezitaja changamoto za walimu nchini  kuwa ni uhaba  wa nyumba za walimu, madai mbalimbali  ya walimu  bado yapo katika halmashauri  pamoja na ajira  kwa walimu huku akiwatoa hofu kuwa madai yote hayo Serikali kwa kushirikiana na CWT yatapatiwa ufumbuzi.

Naye  Kaimu rais wa CWT, Dina Mathamani amesema wao kama walimu wanaipongeza Serikali kwa kuona  umuhimu wa kutoa tuzo na pongezi kwa walimu waliofanya vizuri na kuwafanikisha wanafunzi kufaulu vizuri.

“Ni jambo jema ambalo kila mtu angependa lifanyike,kupitia motisha hii ufaulu unaendelea kupanda siku hadi siku taaluma inapanda na mazingira ya walimu yataendelea kuboreshwa zaidi na kusaidia kila mtu kusimama kwenye nafasi yake,

Kwa niaba ya Chama hiki,naahidi  tutafanya kazi usiku na mchana ,kwa weledi mkubwa  ili kuhakikisha ufaulu wa watoto wetu wapendwa unaongezeka,kupitia hili tutapata wataalamu wabobezi na wajuzi na hatimaye kuwa juu kiuchumi,"amesema.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments