AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUIBA BIBLIA..MWENYEWE AJITETEA ALITAKA TU KUMJUA MUNGUMwanaume ambaye amekamatwa na kushtakiwa kwa kuiba biblia mbili kwenye duka kubwa jijini Nairobi anasema alichokuwa akitaka ni kumjua Mungu tu.

Augustine Wanyonyi, 35, aliambia mahakama kwamba aliiba Biblia hizo ili asome na kumjua Mungu zaidi.Alipoulizwa kwa nini aliiba nakala mbili badala ya moja, alisema Biblia ya pili alikusudia kwa ajili ya mkewe.

Wanyonyi alifika mbele ya Hakimu Mkuu wa mahakama ya Milimani katika Jiji la Nairobi Susan Shitubi ambapo alikiri kutenda kosa hilo.

Niliiba biblia ili nisome, nielewe na kuhubiri neno la Mungu badala ya kujiua kutokana na matatizo yanayonikabili,” Wanyonyi aliambia mahakama. Alishtakiwa mnamo Jumanne tarehe 1 Februari na kurudi mahakamani kuhukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kosa hilo.

Wanyonyi alikamatwa Jumapili baada ya kupatikana na nakala mbili za biblia zenye thamani ya Shilingi 2,100 za Kenya.

Kulingana na ripoti ya polisi iliyosomwa na wakili wa Serikali Alice Mathangani, mshtakiwa alikwenda kwenye duka hilo mwendo wa saa tisa mchana katika tarehe iliyotajwa, na kuiba biblia hizo mbili na kuzificha ndani ya suruali yake.

“Alinaswa na kanda ya CCTV ya duka kuu na baadaye kukamatwa na wahudumu wa CCTV baada ya kushindwa kulipia bidhaa sawa na hiyo alipofika kwa kaunta,” mwendesha mashtaka alisema.


Mwendesha mashtaka pia aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa alikuwa na rekodi ya awali ya wizi wa dukani ambapo alishtakiwa Desemba 2021 lakini akaachiliwa na mahakama nyingine baada ya kuomba msamaha.

Hakimu aliamuru ripoti ya kabla ya hukumu iwasilishwe mahakamani ndani ya siku saba. Atafikishwa mahakamani kuhukumiwa mnamo Februari 16.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post