MKE AKATWA MIKONO KWA SHOKA, SERIKALI YAPIGWA FAINI



Matukio ya ukatili wa jinsia na unyanyasaji, si kwa Waafrika pekee bali ni janga la dunia nzima ambapo mwanamke mmoja kutoka nchini Urusi, Margarita Gracheva mwenye umri wa miaka 26 amesimulia jinsi mumewe alivyomkata mikono kwa shoka.

Tukio hilo limesababisha Mahakama ya Haki za Binadamu ya Jumuiya ya Ulaya (ECHR) kuiamuru serikali ya Urusi, kumlipa mwanamke huyo fidia ya dola za Kimarekani 400,000, sawa na shilingi milioni 900 huku mwanaume aliyefanya ukatili huo, akiendelea kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela aliyohukumiwa.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa Jumanne ya Desemba 14, mwaka huu, sababu za Mahakama ya ECHR kuipiga faini Serikali ya Urusi, ni baada ya uchunguzi kubaini kwamba polisi wa nchi hiyo hawakuchukua hatua stahiki ili kuzuia ukatili huo baada ya kupewa taarifa kutoka kwa mwanamke huyo, kabla ya kutokea kwa tukio hilo.

Sababu nyingine inatajwa kuwa ni sheria za nchi hiyo, kutotoa uzito kwa makosa ya unyanyasaji wa kijinsia ambapo mwaka 2017, serikali ya nchi hiyo ililegeza masharti kwa watu wanaokutwa na hatia ya makosa ya ukatili wa kijinsia na hivyo kuchochea kuongezeka kwa matukio hayo.

Akizungumza na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Margarita amesimulia kisa kizima kilichosababisha mumewe amkate mikono, simulizi ambayo imegusa hisia za watu wengi duniani kote.

Margarita anasema tukio hilo lilitokea Desemba 2017 ambapo mwezi mmoja kabla ya tukio hilo, mwanaume huyo alimtishia kumuua kwa kumuwekea kisu shingoni, akimtuhumu kwamba alikuwa akiisaliti ndoa yao lakini baada ya mwanamke huyo kutoa taarifa polisi, aliambiwa arudi nyumbani wakamalizane kifamilia na mumewe.

Anazidi kueleza kwamba alirudi nyumbani lakini mumewe aliendelea kumtishia kila siku. Siku ya tukio mwanaume huyo alimchukua mkewe na wanaye, baada ya kuwafikisha watoto shule, waliwaacha kisha mwanaume huyo, Dmitry Grachev, aliendesha gari mpaka kwenye msitu uliopo nje ya Jiji la Moscow.

Baada ya kufika kwenye msitu huo, Dmitry alitengeneza michoro kwenye mikono yake kisha akaiweka juu ya gogo la mti na kukata mikono yake yote miwili kwa shoka, hali iliyosababisha apoteze fahamu kutokana na maumivu aliyokuwa akiyasikia, ikiwa ni pamoja na kuvuja damu nyingi.

Inazidi kuelezwa kwamba baada ya kumfanyia ukatili huo mkewe, Dmitry alimpeleka hospitalini akivuja damu na kuwapa madaktari sanduku lililokuwa na mkono wa kulia wa mke wake kisha akaenda kujisalimisha polisi.

Mwanamke huyo anaeleza kwamba wakiwa msituni, alijaribu kupiga kelele za kuomba msaada na kumsihi sana mumewe asimfanyie kitendo hicho lakini alimwambia ageuzie uso wake pembeni, kisha akamkata bila huruma.

Baada ya tukio hilo, mwanaume huyo alishtakiwa kwa utekaji nyara, kutishia kumuua na kumjeruhi mke wake vibaya kwa kumkata mikono ambapo alikiri mashtaka yote na kuhukumiwa kifungo cha miaka 14 jela, adhabu ambayo ilionekana kuwa ndogo ukilinganisha na madhara aliyomsababishia mkewe.

Kesi ya Margarita iliionesha dunia jinsi sheria za Urusi kuhusu unyanyasaji wa kijinsia zilivyokuwa dhaifu, baada ya makosa kadhaa kuondolewa katika kanuni za uhalifu mwaka 2017 chini ya serikali ya Rais Vladimir Putin.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments